Askofu wa
Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, ametoa taarifa rasmi ya
kijimbo kuhusu kifo cha Baba Mtakatifu Fransisko, kilichotekea leo saa
1:37asubuhi kwa saa za Vatikani, sawa na saa 2:35 kwa saa za Afrika
Mashariki.
Kupitia taarifa hiyo, Askofu Sangu amewaomba
Mapadre, watawa na waamini wa Jimbo la Shinyanga kuendelea kumwombea ili Mungu
ampokee katika makazi yake ya milele wakati wakisubiri taarifa ya taratibu za
mazishi kutoka Vatikani.
Askofu Sangu akinukuu maneno ya Karmeli wa Vatikani
Mwadhama Kelvin Kardinali Farrell, amesema Kanisa litaendelea kumkumbuka Baba
Mtakatifu Fransisko kwa majitoleo makubwa kwa utumishi wa Mungu na Kanisa,
akiwafundisha watu wa Mungu kuziishi tunu za Injili kwa umanifu, ujasiri na
upendo kwa ulimwengu wote ikiwemo maskini na wale waliotengwa.
Askofu Sangu amesema yeye binafsi na wanajimbo la
Shinyanga wataendelea kumuenzi na kumkumbuka Papa Fransisko kwa mema mengi
aliyowafanyia , ikiwemo kumpa yeye binafsi hadhi ya umonsinyori wakati akifanya
utume katika Idara ya Uinjulishaji wa watu huko Vatikani na baadaye Aprili 2
mwaka 2021 akumteua kuwa Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga kufuatia kifo cha
Askofu wa tatu wa Shinyanga Hayati Aloysius Balina.
Kifo cha Papa Fransisko aliyekuwa na umri wa miaka 88 ambacho kimetokea kwenye makazi yake ya Casa Santa Marta huko Vatican, kimetangazwa na Camerlengo wa Vatikani (Msimamizi mkuu wa mpito wa shughuli za Vatikani) Mwadhama Kelvin Kardinali Joseph Farrell.
Post a Comment