" BALOZI NCHIMBI: TUSIVURUGWE MIEZI MICHACHE KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

BALOZI NCHIMBI: TUSIVURUGWE MIEZI MICHACHE KUELEKEA UCHAGUZI MKUU

 -Aelekeza RC, Mawaziri wawili kulipa fidia Nyatwali – Bunda


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amewataka Watanzania kuchukua tahadhari dhidi ya wanasiasa wanaojaribu kuhatarisha haki, amani na utulivu wa nchi, huku Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 ukikaribia kwa miezi mitano tu.

Akizungumza na wananchi wa Bunda leo Jumanne, tarehe 22 Aprili 2025, wakati wa ziara yake ya siku tano mkoani Mara, Dkt. Nchimbi alisema kipindi cha uchaguzi huwa na majaribu mengi, ikiwemo uchochezi wa chuki, uhasama na vurugu unaotokana na kauli au matendo ya baadhi ya watu, hasa wanasiasa.

“Mwaka huu mtasikia maneno mengi, hata wasiozoea kusema watajaribu kusema ili kuchonganisha na kuamsha vurugu. Watanzania tuwakatae watu wa aina hiyo. Tusikubali amani yetu iliyodumu tangu uhuru ichezewe ndani ya miezi michache kabla ya uchaguzi,” alisema.

Balozi Nchimbi aliwasifu wananchi wa Bunda kwa kuwa watu wa kazi na maendeleo, akisema: “Ukija kwa watu wa Bunda na kuzungumzia maandamano, wanauliza kwanza kama kuna mkate kwenye maandamano. Taifa zima linapaswa kufikiri hivyo.”

Aidha, aliwahimiza wananchi kuhakikisha wanaboresha taarifa zao kwa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ili waweze kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu.

Katika hatua nyingine, akigusia suala la fidia kwa baadhi ya wakazi wa Nyatwali waliohamishwa kupisha njia ya wanyama, Balozi Nchimbi alimwelekeza Mkuu wa Mkoa wa Mara kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na Wizara ya Fedha kuhakikisha waliobaki wanalipwa ndani ya siku 14.

“Takriban asilimia 90 wameshalipwa. Wanaobakia ni wachache tu, na wengine wanalalamikia kiwango cha fidia. Nimelizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, na nimeelezwa fedha ipo hazina. Namtumia salamu Waziri Mwigulu – hela hiyo itoke,” alisema.

Ziara ya Balozi Nchimbi inajumuisha wilaya za Bunda, Rorya, Musoma, Tarime na Serengeti, na inalenga pia kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020–2025.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi akizungumza na wananchi wa Bunda, aliposimama kuwasalimia, akiwa njiani kuelekea Musoma, Jumanne, tarehe 22 Aprili 2025. Balozi Nchimbi leo ameanza ziara ya siku tano katika maeneo mbalimbali ya wilaya za Mkoa wa Mara.

Post a Comment

Previous Post Next Post