Kiongozi wa Chama Cha ACT Wazalendo Doroth Semu ameeleza kuwa Chama hicho kitashiriki kikamilifu uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba mwaka huu kwenye nafasi zote za Udiwani, Ubunge, Uwakilishi na Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ule wa Zanzibar.
Akizungumza na wanahabari leo Aprili 16, 2025, Vuga visiwani Zanzibar, Semu ameeleza kuwa maamuzi hayo yametokana na tafakuri waliyoifanya, wakibaini kuwa kususia uchaguzi huo Mkuu kutatoa fursa ya kuimarisha hujuma zaidi za dola dhidi ya Demokrasia, akisema uchaguzi huu utakuwa sehemu ya mapambano dhidi ya mageuzi ya mifumo ya uchaguzi nchini.
"Baada ya tafakuri ya kina, Chama chetu ACT Wazalendo kimejiridhisha kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kinahitaji na kwa hakika kitafurahia iwapo vyama makini vya upinzani vitasusia uchaguzi ili kiendeleze hujuma kwa demokrasia nchini. ACT Wazalendo tumegoma kutoa fursa hiyo kwa CCM.
"Uchambuzi wetu pia unaonesha kuwa katika nchi mbalimbali duniani, kususia uchaguzi kumeimarisha hujuma zaidi za dola dhidi ya demokrasia kwa kutoa mwanya wa kupora kwa urahisi sauti ya wananchi. Mifano ya hili inaweza kupatikana kwenye nchi za Kenya (2017), Misri (2018), Ivory Coast (2020), Zanzibar (2015), Venezuela (2018)." Amesema Doroth Semu.
Aidha katika hotuba yake, Semu ameeleza kuwa ACT Wazalendo inashiriki kwenye uchaguzi huo kutokana na kubaini kuwa CCM imeshindwa kuwakomboa watanzania kiuchumi, kisiasa na Kijamii, hivyo ushiriki wao ni jukwaa la vijana, wakulima na wafanyakazi wanaonyonywa, wananchi wanaokandamizwa na wale wanaopuuzwa na kuonewa katika kuiondoa @ccmtanzania madarakani.
Katika hatua nyingine, Chama hicho kimeeleza kuwa bado kinaendeleza mapambano ya kupigania mageuzi ya mifumo ya uchaguzu nchini, akieleza kuwa Viongozi na wanachama wa Chama hicho wapo tayari kulipa gharama za mapambano hayo bila ya kukata tamaa mpaka pale kutakapokuwa na chaguzi za haki, uhuru na zenye kuaminika.
Post a Comment