
Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kanda ya Serengeti leo Aprili 16, 2025
kimetoa tamko mbele ya waandishi wa habari mkoani Shinyanga, kufuatia kikao cha
siku tatu cha kamati tendaji ya kanda hiyo kilichofanyika mjini Shinyanga.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya Serengeti, Lucas Ngoto, amesema kikao hicho
kimepitisha maazimio mbalimbali, huku kikitoa msimamo thabiti wa chama hicho.
“Kitendo
cha serikali kumfungulia kesi ya uhaini Tundu Lissu ambaye ni mwenyekiti wetu
wa CHADEMA Taifa tunakichukulia kama ni hofu ya uchaguzi. Tunalilaani vikali
tukio hilo na tunaitaka serikali ya Chama cha Mapinduzi imwachie mwenyekiti
wetu mara moja,” amesema Ngoto.
Ameongeza
kuwa kuanzia sasa, kanda ya Serengeti itakuwa na ajenda mbili kuu kuelekea
uchaguzi mkuu wa 2025.
“Ninawaasa
wanachama wa CHADEMA kanda ya Serengeti na Watanzania kwa ujumla kuwa ajenda
yetu ya kwanza itaendelea kuwa ‘No Reform, No Election’, lakini kuanzia leo
tunaitangaza rasmi ajenda yetu ya pili kuwa ‘Free Tundu Lissu’. Serikali ya CCM
wasidhani kutufunga mikono, tutasimamia madai yetu hadi mwisho,” amesema.
Viongozi wa mikoa ya Mara, Simiyu na Shinyanga waliokuwepo katika kikao hicho pia wameeleza kuunga mkono jitihada za chama hicho katika kudai mabadiliko ya msingi ya mfumo wa uchaguzi, wakisema kuwa wako tayari kushiriki kikamilifu katika kampeni za kuhamasisha wananchi kudai haki zao za kidemokrasia.
Mwenyekiti
wa CHADEMA kanda ya Serengeti, Lucas
Ngoto, akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 16, 2025.
Post a Comment