CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimepewa siku 21 na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, kuwasilisha utetezi wake mahakamani hapo wa maandishi (written statement of defence - WSD) katika kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa raslimali na uendeshaji, inayowakabili.
Kwa maana hiyo chama hicho kimeamuriwa kuwasilisha mahakamani hapo utetezi wake huo kabla au mpaka kufikia Mei 9, 2025.
Amri hiyo imetolewa leo Aprili 17 2025 Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi hiyo, ilipotajwa kwa mara ya kwanza.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, ambaye anajitambulisha kama mwanachama na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa chama hicho, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu, ambao wanajitambulisha na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chama hicho.
Katika kesi hiyo, mshtakiwa wa kwanza ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema huku Katibu Mkuu wa Chadema, akiwa mshtakiwa wa pili.
Mawakili waliowakilisha Chadema ni Jeston Justine na John Chogomo wameiomba mahakama iwape muda wa siku 21 kuandaa na kuwasilisha utetezi wake, Kwa mujibu wa Sheria.
Wakili wa wadai, Shaban Marijani hakuwa na pingamizi dhidi ya ombi hilo na Jaji Mwanga pia akaridhia.
" Maombi ya upande wa wadaiwa yamekubaliwa na wanapewa siku 21 kutoka leo (Aprili, 17,2025) kuwasilisha utetezi wake. Hivyo wadaiwa mnaelekezwa kuwasilisha mahakamani utetezi wenu kufikia au kabla ya Mei 21, 2025", amesema Jaji Mwanga.
Pia Jaji Mwanga amepanga kuwa kesi hiyo itatajwa tena mahakamani hapo Mei 12, 2025, kwa ajili ya kuangalia kama maelekezo hayo yatakuwa yamekamilika na Kwa ajili ya amri nyingine muhimu.
Katika kesi ya msingi, walalamikaji wanaiomba Mahakama itamke na kuamuru kuwa wadaiwa wamekiuka sheria zinazohusiana na vyama vya siasa na Katiba ya chama hicho wakidai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara;
Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Walalamikaji pia wameiomba Mahakama itoe hukumu na amri dhidi ya wadaiwa kwamba wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili na hivyo Mahakama itamke na kuwaelekeza wadaiwa kuzingatia kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019.
Pia walalamikaji wanaomba kusitishwa kwa muda kwa shughuli zote za kisiasa hadi hapo kutakapokuwepo na utekelezaji wa maagizo ya Mahakama.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itoe amri ya zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi Wajibu Maombi watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na pia iamuru , wadaiwa walipe gharama za kesi hiyo na itoe nafuu nyingine yoyote ambayo Mahakama itaona inafaa kuzitoa.
Post a Comment