" JUKWAA LA UTALII WA CHAKULA DUNIANI KUFANYIKA TANZANIA-MHE. MAJALIWA

JUKWAA LA UTALII WA CHAKULA DUNIANI KUFANYIKA TANZANIA-MHE. MAJALIWA

 


Na John Mapepele

Jukwaa la Pili la Utalii wa Chakula Duniani kwa Kanda ya Afrika linaloandaliwa na Shirika la Utalii Duniani linatarajiwa kufanyika hapa nchini Aprili mwaka huu jijini Arusha.

Haya yamebainishwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa alipokuwa akiwasilisha mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya waziri mkuu na ofisi ya bunge kwa mwaka 2025/2026 bungeni jijini Dodoma.
Pia amesema Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) yaliyopangwa kufanyika Agosti, 2025 ni fursa nyingine adhimu ya kutangaza vivutio vyetu vya utalii ikizingatiwa kuwa michezo huhusisha mashabiki wengi kutoka nchi mbalimbali ambapo ametoa rai kwa watanzania kutumia vema fursa hiyo adhimu.

Aidha, Mhe. Majaliwa amefafanua kuwa katika mwaka 2024/2025, utalii wa mikutano na matukio umekuwa kwa kiwango cha juu ambapo mikutano mbalimbali ya kimataifa ilifanyika nchini ikiwemo Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika Januari, 2025.

Pia amesema Taasisi ya World Travel Awards imeitambua Tanzania kama eneo linalovutia zaidi kiutalii kwa mwaka 2024. Vilevile, eneo linaloongoza kwa utalii wa safari Dunia kwa mwaka 2024; Hifadhi ya Taifa Serengeti kuendelea kuwa bora duniani kwa miaka sita (6) mfululizo; na Mlima Kilimanjaro kuwa kivutio bora cha utalii barani Afrika kwa mwaka 2024.

Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kukuza utalii na kuendeleza maliasili zilizopo nchini ili kuiwezesha nchi kupata mapato na kukuza ustawi wa wananchi. Katika mwaka 2025/2026, Serikali itaendelea kutangaza utalii wa ndani na nje ya nchi; kuibua na kuendeleza mazao ya utalii ya kimkakati na kuimarisha usimamizi mifumo ya ukusanyaji wa mapato yatokanayo na shughuli za utalii na uhifadhi.

Post a Comment

Previous Post Next Post