" JUMUIYA YA WAZAZI CCM MKOA WA SHINYANGA YAZINDUA WIKI YA WAZAZI KWA KISHINDO KISHAPU

JUMUIYA YA WAZAZI CCM MKOA WA SHINYANGA YAZINDUA WIKI YA WAZAZI KWA KISHINDO KISHAPU

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala Mlolwa, akizungumza kwenye uzinduzi wa wiki ya Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga leo Aprili 9, 2025.


Na Mapuli Kitina Misalaba

Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga leo Aprili 9, 2025 imezindua rasmi wiki ya wazazi kwa kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo, kupanda miti na kufanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Shule ya Sekondari Bunambiyu Wilaya ya Kishapu.

Mgeni rasmi katika uzinduzi huo ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala Mlolwa, ambaye pamoja na kutoa hotuba ya kuhimiza malezi bora, ushiriki wa wazazi katika maendeleo na mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi mkuu, ametembelea shule hiyo na kukagua miradi iliyotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano.

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, Mhe. Mlolwa ameipongeza Jumuiya ya Wazazi kwa kuandaa maadhimisho hayo muhimu ambayo amesema yanadhihirisha namna wazazi wanavyoshiriki kikamilifu katika kuimarisha chama na jamii kwa ujumla.

“Jumuiya ya wazazi imeendelea kuwa nguzo muhimu ndani ya CCM, si tu kwa ushauri bali pia kwa kukemea maovu na kusimamia maadili,” amesema Mlolwa.

Aidha, amempongeza Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Shinyanga, John Siagi, kwa kuongoza vyema jumuiya hiyo na kuifanya kuwa mfano wa kuigwa katika mkoa.

Mlolwa ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM akibainisha kuwa mkoa wa Shinyanga umepokea miradi mingi ya maendeleo katika kila kata na kijiji, jambo ambalo limechochea ustawi wa wananchi kiuchumi na kijamii.

Amesema kuwa katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2025, CCM Mkoa wa Shinyanga itahakikisha mgombea urais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza wake Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi wanashinda kwa kishindo, huku akisisitiza kuwa Shinyanga itaibuka kinara wa kura za ndiyo kwa nchi nzima.

Aidha, Mlolwa amewahimiza wananchi kuchagua viongozi bora wenye maono na uwezo wa kutatua changamoto zao, akionya dhidi ya wagombea wanaotumia rushwa kutafuta uongozi. “Wajumbe hakikisheni mnapitisha wagombea wanaokubalika kwa wananchi. CCM haitatoa jina la mgombea anayekubalika”.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Shinyanga, John Siagi, amesema tayari wameandaa mpango kazi kuelekea uchaguzi mkuu wenye lengo la kuhakikisha CCM inapata ushindi wa kishindo.

Pia amewahimiza wazazi kutumia wiki hiyo kutoa taarifa za vitendo vya ukatili wa watoto ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Siagi amekemea mmomonyoko wa maadili miongoni mwa watoto na vijana, akiwataka wazazi na walezi kuwalea watoto katika maadili ya kitanzania. “Tukiwalea watoto wetu katika misingi bora ya maadili tutakuwa na taifa la watu wasomi, waadilifu na wenye kujali utu,” amesema Siagi.

Katika hatua nyingine ya uzinduzi huo, Mhe. Mabala Mlolwa ametembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika shule ya sekondari Bunambiyu ambapo Mkuu wa shule hiyo, Mzee Matata Joel, ameeleza kuwa serikali kupitia awamu ya sita imetoa zaidi ya shilingi milioni 166.4 katika kipindi cha miaka mitano.

Kwa mujibu wa Mzee Matata, fedha hizo zimetumika kujenga vyumba vya madarasa, ofisi, pamoja na matundu ya vyoo ambapo hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 165.8 zimetumika kwa mafanikio makubwa.

Baada ya ukaguzi huo, viongozi wa CCM wakiongozwa na Mhe. Mlolwa walipanda miti katika eneo la shule hiyo ikiwa ni ishara ya utunzaji wa mazingira na kuhamasisha jamii katika suala la mazingira.

Viongozi wengine walioshiriki katika uzinduzi huo ni pamoja na Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Odilia Batimayo; Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo, Richard Masele; Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Anord Makombe, pamoja na viongozi wengine wa chama na jumuiya zake.

Maadhimisho ya wiki ya wazazi ngazi ya mkoa yanaendelea kwa kutoa elimu kwa wazazi juu ya malezi bora, afya, elimu, maadili, pamoja na kujadili masuala muhimu ya maendeleo ya jamii.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala Mlolwa, akizungumza kwenye uzinduzi wa wiki ya Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Shinyanga leo Aprili 9, 2025.



 

Post a Comment

Previous Post Next Post