" JUMUIYA YA WAZAZI CCM YATIMIZA MIAKA 70! KATIBU DORIS KIBABI ACHEMSHA MOTO KWA KAULI ZAKE SHINYANGA!

JUMUIYA YA WAZAZI CCM YATIMIZA MIAKA 70! KATIBU DORIS KIBABI ACHEMSHA MOTO KWA KAULI ZAKE SHINYANGA!

 

Na Daniel Sibu, Misalaba Media

Shinyanga, Aprili 11, 2025 Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Shinyanga Mjini imeadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake kwa kufanya shughuli ya upandaji miti katika Shule ya Msingi Mapinduzi B, iliyopo kata ya Ngokoro, pamoja na kikao maalum cha kujadili mustakabali wa chama kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani ya chama mwaka huu.

Katibu wa Jumuiya hiyo wilaya ya Shinyanga Mjini, Bi. Doris Kibabi, amesema kuwa sherehe hizi ni ukumbusho wa mchango mkubwa wa Jumuiya ya Wazazi katika sekta za elimu, malezi, afya na mazingira.

“Leo tupo hapa kupanda miti kama alama ya ukumbusho wa miaka 70 ya Jumuiya yetu, lakini pia tunachangia mazingira bora kwa watoto wetu mashuleni kwa kuwapatia kivuli na hewa safi,” alisema Bi. Doris.

Akiwahutubia wanajumuiya na wananchi waliohudhuria, Bi. Doris alisisitiza kuwa mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi ndani ya chama, na hivyo wanachama wanapaswa kujitathmini kabla ya kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali.

“Form zinatoka tarehe 1 Mei, huu ni wakati wa kujitathmini na kujiuliza kama unafaa. Chama sasa kinataka wagombea safi, wenye uwezo na wanaokubalika kwa wananchi. Hakuna nafasi kwa watu wa ‘makando kando’,” alisisitiza.

Aidha, aliwataka wanaCCM kuepuka migogoro ya ndani kwa kuhakikisha wanaafikiana kabla ya kuchukua fomu katika maeneo yenye mgombea zaidi ya mmoja kutoka jumuiya au kata moja.

“Tukikosa umoja, tutakosa kura. Tuwe na nidhamu, tukubali maamuzi ya chama na tuwape ushirikiano wale waliopitishwa na vikao halali,” alisema.

Katika kikao hicho, alieleza pia kuwa chama kimeweka utaratibu mpya ambapo wagombea watapitia mchujo wa awali kabla ya majina yao kupelekwa katika Halmashauri Kuu ya CCM kwa uamuzi wa mwisho.

Bi. Doris alihitimisha kwa kuhimiza mshikamano, akisisitiza kuwa wanachama wote waendelee kuwa kitu kimoja, waache malumbano, na waendelee kuijenga Jumuiya ya Wazazi pamoja na CCM kwa ujumla.

“Tukisimama pamoja, tutapata viongozi bora, wanaojali wananchi na wenye uwezo wa kutatua shida za watu wetu. Wiki ijayo tunaanza usajili wa wanachama, karibuni kwa wingi mjisajili na kupata kadi zenu papo hapo,” alihitimisha.

 






























Post a Comment

Previous Post Next Post