" KAMANDA MAGOMI ATOA SALAAMU ZA PASAKA, AELEZA MIKAKATI YA ULINZI MKALI MKOANI SHINYANGA

KAMANDA MAGOMI ATOA SALAAMU ZA PASAKA, AELEZA MIKAKATI YA ULINZI MKALI MKOANI SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, amewatakia heri ya sikukuu ya Pasaka wakristo na wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga, huku akibainisha kuwa jeshi la polisi limejipanga kikamilifu kuhakikisha amani na usalama vinatawala katika kipindi chote cha maadhimisho ya sikukuu hiyo takatifu.

Akizungumza na Misalaba Media leo Jumamosi Aprili 19, 2025, Kamanda Magomi amesema jeshi lake limeimarisha ulinzi katika maeneo yote muhimu ikiwemo makanisa, barabarani na katika maeneo ya burudani, ili kuhakikisha wakazi wa Shinyanga wanaadhimisha Pasaka kwa amani na utulivu.

Ameeleza kuwa mikakati madhubuti ya kiusalama imeandaliwa na kutekelezwa katika Halmashauri zote sita za Mkoa wa Shinyanga, ambazo ni Manispaa ya Shinyanga, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Kishapu, Ushetu, Kahama na Msalala, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha askari wapo tayari muda wote kuhakikisha hakuna uvunjifu wa amani.

“Tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba tunasimamia na kuimarisha shughuli zote za ulinzi na usalama kuanzia mkesha wa Pasaka leo Jumamosi. Katika makanisa yote tumejipanga vizuri, na hilo ni jukumu letu la msingi,” amesema.

Kamanda huyo amewaasa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wapo salama wakati wa kusherehekea Pasaka, akisisitiza marufuku ya disko toto, ambayo mara nyingi huwa chanzo cha madhara kwa watoto.

“Nisisitize kwamba disko toto hapana, nimepiga marufuku. Watoto kama ni kanisani waende, lakini wazazi wanaweza kuwaambatana na watoto kuwapeleka kwenye sehemu nzuri za kubembea au kupumzika wakiwa pamoja, ili kuhakikisha usalama wao,” amesema.

Aidha, Kamanda Magomi ametoa wito kwa madereva wa vyombo vya moto, hususan bodaboda, waendesha guta, pamoja na watembea kwa miguu, kuheshimu sheria za usalama barabarani ambapo ameonya kuwa jeshi la polisi halitasita kuchukua hatua kali kwa wote watakaokiuka sheria, hasa wale watakaokuwa wakitumia vilevi wakati wa kuendesha vyombo vya moto.

“Sisi tupo barabarani masaa 24 kuhakikisha hawatumii vilevi wakati wa kuendesha vyombo vya moto. Tunataka sherehe hizi zisherehekewe kwa amani na utulivu,” amesisitiza.

Mwisho, Kamanda Magomi amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Shinyanga kwa ushirikiano wanaoutoa kwa jeshi la polisi, na kuwatakia Pasaka njema.

“Nawashukuru sana wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga kwa ushirikiano mkubwa wanaolipa jeshi la polisi katika kuhakikisha kwamba amani na utulivu vinatawala. Nawatakieni nyote Pasaka njema, na Mungu awabariki sana.”

Post a Comment

Previous Post Next Post