" KAMATI YA PAC YARIDHISHWA UJENZI BWAWA LA MEMBE

KAMATI YA PAC YARIDHISHWA UJENZI BWAWA LA MEMBE









NIRC Dodoma.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali imeridhishwa na utekelezaji wa ujenzi mradi wa bwawa la Umwagiliaji Membe lililopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma.

Kamati hiyo imesema, ujenzi wa bwawa umeendana na thamani ya fedha iliyowekwa.

Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika mradi wa wa bwawa la Membe Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, amesema kamati hiyo imeridhishwa na ujenzi huo kwani thamani ya fedha unaendana na ujenzi.

“Si tu kujenga bwawa bali ni kuhakikisha bwawa hilo linatumika katika shughuli zote za Umwagiliaji wa mashamba na kuleta tija katika kilimo,”amesema.

Amesisitiza kuwa, kukamilika kwa mradi wa bwawa la Membe kutaongeza uzalishaji wa mazao hivyo Wizara ya Kilimo ina wajibu kuhakikisha wakulima wanapata uhakika wa masoko ili kuepuka changamoto zitakazojitokeza.

Mhe. Kaboyoka ameishauri Tume kutoa elimu kwa wakulima kupanda miti katika eneo hilo, ili kukabiliana na hali ya ukame iliyopo mkoani Dodoma.

Baadhi ya wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo akiwemo Mhe. Aloyce Kamwelwe wameipongeza Tume kwa kuwa na weledi katika usimamizi wa mradi na kuhakikisha unazingatia viwango vya ubora vilivyopo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) Bw. Raymond Mndolwa, amesema mradi wa ujenzi bwawa la Membe umefikia asilimia 87.5% ya utekelezaji.

Amesisitiza kuwa ujenzi wa Bwawa hilo la Membe litakuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita za ujazo bilioni 12.

“Maji haya yataweza kumwagilia hekta 2,500 za mashamba kwa wakulima zaidi ya 1,500 wa kata ya Membe,”amesema.

Nao baadhi ya wakulima wa Membe akiwemo Jemima Kalebi, wameishukuru Serikali kupitia Tume kwa hatua ya utekelezaji wa mradi huo kwani unaleta matumaini.

Jemima amesema, wana matarajio makubwa katika kilimo cha Umwagiliaji kuwa kitainua uchumi wao na kuwa na uhakika wa chakula.

Post a Comment

Previous Post Next Post