Na Mwandishi Wetu - Singida
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi ametoa wito kwa Waajiri na Vyama vya Wafanyakazi kuweka msukumo kwa wafanyakazi kushiriki katika michezo ili kuimarisha afya zao.
Mhe. Katambi ameyasema leo Aprili 22, 2025 katika viwanja vya CCM Liti mkoani Singida wakati wa akifungua michezo ya Mei Mosi Taifa 2025 yenye kauli “Michezo kwa Afya, Ajira, Furaha, na Kazi Inaendelea. Wafanyakazi Tushiriki vyema Uchaguzi wa 2025 Tupate Viongozi Bora. Mshikamano Daima”
"Michezo ni Afya na njia nzuri ya kujenga umoja na mahusiano mema mahali pa kazi, hivyo kuwa na afya bora kutawawezesha kutoa huduma nzuri kwa wananchi” amesema
Aidha Mhe. Katambi amempongeza Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuwa chachu ya mafanikio makubwa katika sekta ya michezo ikiwemo kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo katika maeneo mbalimbali nchini.
“Jitihada za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeleta mafanikio katika michezo nchini tumeshuhudia hali ilivyo katika mchezo wa mpira wa miguu kupitia Goli la Mama namna lilivyowajenga wachezaji kuwa na hamasa” amesema.
Kadhalika, Naibu Waziri Katambi ametoa rai kwa waajiri kuhakikisha wanatenga muda kwa watumishi kufanya mazoezi na hivyo kujiepusha na magonjwa yanayoweza kuepukika.



Post a Comment