" KAZIMOTO AMOS AFARIKI DUNIA BAADA YA KUNYWA SUMU YA PANYA SHINYANGA

KAZIMOTO AMOS AFARIKI DUNIA BAADA YA KUNYWA SUMU YA PANYA SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Kijana mmoja anayefahamika kwa jina la Kazimoto Amos mwenye umri wa Miaka 27, mkazi wa mtaa wa Sanjo, kata ya Chamaguha, Manispaa ya Shinyanga, amefariki dunia baada ya kunywa sumu ya panya.

Akizungumza na Misalaba Media kwa niaba ya familia, kaka wa marehemu, Peter Ibrahim Richard, amesema kuwa tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana ambapo Kazimoto alimweleza kwa njia ya simu kuwa tayari amekunywa sumu na alikuwa katika hali mbaya.

"Alinipigia simu na kuniambia kuwa amekunywa sumu ya panya na muda wowote anafariki. Mimi nilikuwa Maganzo nilitoa taarifa haraka nyumbani, wakafika chumbani kwake wakamkuta hali yake ni mbaya, pia walipiga simu kwa mwenyekiti wa mtaa na wakawashirikisha majirani kumpa huduma ya kwanza," amesema Peter.

Baada ya juhudi hizo, Kazimoto alikimbizwa kwenye zahanati ya Chamaguha lakini alifariki dunia wakati akihudumiwa na wahudumu wa afya.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Sanjo, Bwana Moshi Ngoyeji, ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kuchukua maamuzi ya kujiua wanapokutana na changamoto mbalimbali za maisha.

"Ni muhimu watu kutafuta msaada na kushauriana na wengine wakati wanapopitia magumu badala ya kufikia hatua ya kuamua kuondoa uhai wao," amesema Mwenyekiti huyo.

Mazishi ya Kazimoto Amos yanatarajiwa kufanyika leo Alhamisi katika mtaa wa Sanjo, Chamaguha Manispaa ya Shinyanga.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post