Na WAF, KILIMANJARO
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) imepongezwa kwa kuendelea kuimarisha huduma za Optometria zinazotolewa katika Idara ya Macho huku ikishauriwa kuimarisha huduma zake na kufikia kuwa kituo cha umahiri.
Pongezi hizo zimetolewa Aprili 14,2025 na timu ya Usimamizi Shirikishi inayoongozwa na Msajili Baraza la Optometria Bw. Sebastiano Millanzi.
"Uwepo wa huduma maalum za optometria mnazozitoa Idarani hapa zikiwemo huduma za Optometria kwa Watoto _(Pediatric Optometry),_ Kupima na kurekebisha Uono hafifu _(Low Vision Assessment and Rehabilitation)_ na Huduma za kupima na kurekebisha makengeza _(Orthoptics),_ ni dhahiri kwamba mnastahili kuwa kituo cha umahiri," amesema Bw. Millanzi.
Bw. Millanzi amesema KCMC ina nafasi ya kipekee ya kuwa kitovu cha ubora katika huduma za macho kwa kutumia rasilimali zilizopo, ikiwa ni pamoja na miundombinu, wataalam waliobobea na historia yake katika kutoa huduma bora za afya.
Bw. Millanzi ametumia fursa hiyo kuwaasa wataalam wa Optometria kujiendeleza kwenye mafunzo ya muda mfupi kati ya miezi mitatu (3) mpaka sita (6) yanayotolewa hospitalini hapo ili waweze kuwasaidia wananchi kupata huduma bora.
Mapema Mganga Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Jerry Khanga, akiikaribisha timu hiyo mkoani hapo, ameiomba timu ya usimamizi kuhakikisha inafanya usimamizi wa kina na wa kitaalamu ili taarifa watakayopata iweze kuusaidia mkoa kubaini maeneo yenye changamoto na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha huduma hizo.
Dkt. Khanga amesema, taarifa sahihi na ya kina kutoka kwa timu hiyo ni muhimu kwa mkoa ili kupanga maendeleo ya sekta ya afya hasa katika eneo la macho ambalo linahitaji maboresho ya kiufundi na kimkakati.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa mashirikiano kati ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na wadau wa sekta ya afya ili kuhakikisha huduma za macho zinaimarika na kuwa bora zaidi kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro na maeneo jirani.
Ziara hiyo imehusisha wataalam kutoka Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na mkoa ikiwa na lengo la kufanya tathmini ya hali ya utoaji wa huduma za macho na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.
Post a Comment