Na Mapuli Kitina Misalaba
Kijana mmoja anayefahamika kwa jina Joseph Emmanuel Ndulu mwenye umri wa Miaka 22, mkazi wa mtaa wa Bugweto kata ya Ibadakuli manispaa ya Shinyanga, amefariki dunia baada ya kudumbukia katika mto Mhumbu eneo la Chamaguha wakati akifanya shughuli ya kulowa samaki.
Akizungumza na Misalaba Media, Mwenyekiti wa mtaa wa Chamaguha, Bwana Husein
Matamba, ameeleza kuwa tukio hilo limetokea Ijumaa Aprili 18, 2025, majira ya
saa kumi na moja jioni baada ya kijana mmoja wa mtaa huo kufika na kutoa
taarifa kuwa kuna kijana amedumbukia mtoni.
“Nilifuatwa na kijana mkazi wa mtaa
wangu akanieleza kuwa kuna kijana amedumbukia kwenye mto Mhumbu akiwa analoweka
samaki. Tukaongozana naye hadi mtoni, lakini hatukuona chochote. Niliwaambia
vijana waingie sehemu maji siyo mengi, wakaingia na kweli wakamuona.
Nikawaambia wamtoe. Baada ya kumtoa watu wakamtambua ndipo nikawapigia simu
polisi,” amesema Bw. Matamba.
Ameongeza kuwa baada ya kutoa taarifa kwa polisi,
alimtaarifu pia baba mzazi wa marehemu ambaye alieleza kuwa kijana huyo alikuwa
na tatizo la kifafa kwa muda mrefu.
“Polisi walifika, wakafanya uchunguzi
wao wa awali kisha wakausafirisha mwili wa marehemu kwenda mochwari. Kama
uongozi, tunatoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuchukua tahadhari kubwa
kwa watu wenye matatizo ya kiafya kama haya. Tusiwaache waende mtoni peke yao,”
amesisitiza.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa eneo hilo limekuwa
likishuhudia matukio ya watu kutumbukia mtoni na hivyo ametoa rai kwa wazazi
kuwa na tabia ya kuwakataza watoto wao kuepuka maeneo ya mito bila uangalizi.
Mazishi ya kijana huyo yanatarajiwa kufanyika kesho Aprili
20, 2025 katika mtaa wa Bugweto, kata ya Ibadakuli.
Post a Comment