" KIJANA AFARIKI DUNIA BAADA YA KUTUMBUKIA MTONI AKILOA SAMAKI SHINYANGA

KIJANA AFARIKI DUNIA BAADA YA KUTUMBUKIA MTONI AKILOA SAMAKI SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Kijana mmoja anayefahamika kwa jina Joseph Emmanuel Ndulu mwenye umri wa Miaka 22, mkazi wa mtaa wa Bugweto kata ya Ibadakuli manispaa ya Shinyanga, amefariki dunia baada ya kudumbukia katika mto Mhumbu eneo la Chamaguha wakati akifanya shughuli ya kulowa samaki.

Akizungumza na Misalaba Media, Mwenyekiti wa mtaa wa Chamaguha, Bwana Husein Matamba, ameeleza kuwa tukio hilo limetokea Ijumaa Aprili 18, 2025, majira ya saa kumi na moja jioni baada ya kijana mmoja wa mtaa huo kufika na kutoa taarifa kuwa kuna kijana amedumbukia mtoni.

“Nilifuatwa na kijana mkazi wa mtaa wangu akanieleza kuwa kuna kijana amedumbukia kwenye mto Mhumbu akiwa analoweka samaki. Tukaongozana naye hadi mtoni, lakini hatukuona chochote. Niliwaambia vijana waingie sehemu maji siyo mengi, wakaingia na kweli wakamuona. Nikawaambia wamtoe. Baada ya kumtoa watu wakamtambua ndipo nikawapigia simu polisi,” amesema Bw. Matamba.

Ameongeza kuwa baada ya kutoa taarifa kwa polisi, alimtaarifu pia baba mzazi wa marehemu ambaye alieleza kuwa kijana huyo alikuwa na tatizo la kifafa kwa muda mrefu.

“Polisi walifika, wakafanya uchunguzi wao wa awali kisha wakausafirisha mwili wa marehemu kwenda mochwari. Kama uongozi, tunatoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuchukua tahadhari kubwa kwa watu wenye matatizo ya kiafya kama haya. Tusiwaache waende mtoni peke yao,” amesisitiza.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa eneo hilo limekuwa likishuhudia matukio ya watu kutumbukia mtoni na hivyo ametoa rai kwa wazazi kuwa na tabia ya kuwakataza watoto wao kuepuka maeneo ya mito bila uangalizi.

Mazishi ya kijana huyo yanatarajiwa kufanyika kesho Aprili 20, 2025 katika mtaa wa Bugweto, kata ya Ibadakuli.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post