
Na Mapuli Kitina Misalaba
Kijana mwenye umri wa miaka 16 anayefahamika kwa jina
la Kulwa Yusuph Bukulu amefariki dunia kwa kujinyonga katika kijiji cha
Mwang’osha, kata ya Nyamalogo, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
Tukio hilo limetokea Aprili 11, 2025 majira ya saa
nne asubuhi, ambapo taarifa zake zimethibitishwa na Mwenyekiti wa kijiji cha
Mwang’osha, Magina Lugembe, alipokuwa akizungumza na Misalaba Media.
“Baada ya kupata taarifa za tukio hili nilifika eneo
la tukio na kukuta kweli kijana huyo amejinyonga. Niliwajulisha viongozi
mbalimbali wakiwemo askari wa jeshi la polisi ambao walifika eneo hilo na
kuanza uchunguzi,” amesema Lugembe na kufafanua kuwa marehemu alikuwa akiishi
kwa ndugu yake kijijini hapo.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi,
amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kueleza mazingira ya tukio.
“Ni
kweli, tulipokea taarifa za kijana aitwaye Kulwa Yusuph Bukulu kuwa amejinyonga
hadi kufa. Jeshi la polisi lilifika eneo la tukio na kukuta marehemu
amejinyonga kwa kutumia kamba iliyofungwa kwenye kenchi ya stoo ya pumba za
mifugo,” amesema SACP Magomi.
Ameongeza kuwa baada ya taratibu zote za uchunguzi
wa kitabibu kukamilika, mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili
ya maziko yaliyofanyika Aprili 13, 2025.
Kamanda Magomi ametoa wito kwa jamii kuendelea
kushirikiana na jeshi la polisi katika kutoa elimu ya kujitambua kwa vijana.
“Ni
tukio la kusikitisha sana. Kwa haraka unaweza kuona kijana huyu alikuwa amekata
tamaa. Tunaendelea kutoa elimu kupitia polisi jamii na viongozi wa dini kwa
imani zao tofauti kuhimiza watu kutorudi nyuma au kujitoa uhai wao pindi
wanapopitia changamoto. Siyo sahihi kujinyonga kwa sababu ya kukata tamaa,”
amesema SACP Magomi.
Jeshi la polisi limeeleza kuwa lingeweza kumchukulia
hatua kijana huyo kwa kosa la kujaribu kujiua iwapo angekuwa hai, na hivyo
limehimiza jamii kuwa makini na matukio ya aina hiyo ili kuokoa maisha ya
vijana.
Post a Comment