JUMAPILI hii Aprili 20, 2025, Simba SC itaikaribisha Stellenbosch FC katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Kisiwani Unguja, rekodi zinaonyesha upande mmoja kuwa mtamu zaidi kwa Simba, huku pia ikiwa mchungu pindi inapocheza dhidi ya timu kutoka Afrika Kusini.
Hii itakuwa mara ya nne Simba kukutana na timu kutoka Afrika Kusini katika mashindano ya CAF huku ikiwa na rekodi nzuri inapocheza uwanja wa nyumbani kwani haijawahi kupoteza ikishinda mara zote tatu zilizopita.
Mbali na kuwa na rekodi nzuri ya kushinda nyumbani, lakini Simba imeiondosha mara moja tu timu ya Sauzi katika mtoano huku nyingine ikishindwa kupenya.
Hiyo inaifanya Simba kuwa na mtihani mzito mbele ya Stellenbosch kwani licha ya rekodi yao nzuri ya nyumbani kuwabeba, lakini inahukumiwa na rekodi ya jumla kwa kuvuka hatua inayofuata.
Katika mara tatu Simba ilipocheza nyumbani dhidi ya timu kutoka Afrika Kusini, ilishinda kwa penalti 9-8 dhidi ya Santos kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003.
Mikwaju hiyo ya penalti iliivusha Simba ambayo ilikwenda kukutana na Zamalek na kuiondosha pia, kisha ikafuzu makundi.
Katika michezo miwili ya mtoano dhidi ya Santos, ilianzia ugenini Aprili 13, 2003 matokeo yakiwa 0–0, kisha marudiano nyumbani ikawa 0-0, ndipo penalti zikaivusha Simba.
Baada ya hapo, Mei 15, 2021, Simba ilikutana na Kaizer Chiefs katika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ugenini ilipoteza kwa mabao 4–0, kisha nyumbani Mei 22, 2021 ikashinda 3–0 kwa mabao mawili ya John Bocco dakika ya 24 na 56, huku Clatous Chama akifunga moja dakika ya 86.
Licha ya ushindi huo wa nyumbani, lakini haikutosha Simba kuvuka kwenda nusu fainali kufuatia matokeo ya jumla kuwa 4-3.
Aprili 17, 2022, Simba ilikutana na Orlando Pirates katika mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Simba ilianzia nyumbani na kushinda bao 1-0 lililofungwa na Shomari Kapombe dakika ya 68 kwa penalti, ugenini Aprili 24, 2022, Simba ikafungwa 1-0, ikafanya matokeo ya jumla kuwa sare ya 1-1.
Simba ilipoteza kwa mikwaju 4-3, huku wachezaji wake wawili, Jonas Mkude na Henock Inonga Baka wakikosa penalti. Pia ilishuhudiwa mshambuliaji wa Simba, Cris Mugalu akionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 58.
Post a Comment