" MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZAZI: JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA MBOGWE IMEENDELEA KUTAMBUA MICHANGO YA WAZAZI KATIKA MAENDELEO YA NCHI

MAADHIMISHO YA SIKU YA WAZAZI: JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA MBOGWE IMEENDELEA KUTAMBUA MICHANGO YA WAZAZI KATIKA MAENDELEO YA NCHI

NA ANTHONY SOLLO MBOGWE.

Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita chini ya Mwenyekiti wake Mh Khalima Hassan Chembemoyo imeadhimisha Siku ya Wazazi kwa kutambua mchango mkubwa kutoka kwa wanachama wa Jumuiya hiyo.

Akihutubia wanachama wa Jumuiya hiyo,Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mh Khalima Hassan Chembemoyo amewataka Viongozi wa Jumuiya hiyo kutafuta takwimu za Watoto wasioenda Shule ili zipelekwe kwa Mkuu wa Wilaya ili zifanyiwe kazi ikiwa ni mkakati wa kukabiliana na Adui ujinga katika Wilaya hiyo na kuipeleka mbele Elimu.

Maadhimisho hayo yalifanyika katika viwanja vya Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe,ambapo viongozi mbalimbali wa Jumuiya hiyo iliyoko chini ya Chama cha Mapinduzi CCM,pamoja na wananchi kutoka maeneo mbalimbali Mkoani Geita,walikusanyika kuadhimisha siku hiyo.

Pamoja na kusherehekea Viongozi hao walisisitiza kuwa moja ya majukumu ya Jumuiya hiyo ni kutambua jukumu la wazazi katika Malezi, Elimu, na Ustawi wa Watoto.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mbogwe ,Mh Khalima Hassan Chembemoyo,alisema kuwa wazazi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha mafanikio ya familia na Taifa kwa ujumla.

“Wazazi ndiyo wanaotoa malezi bora na kuwekeza katika watoto wetu,hivyo kuwa na mchango mkubwa katika ustawi wa jamii katika siku hii ya leo,tunawatambua na kuwashukuru kwa juhudi zao zisizo na kifani,”alisema Chembemoyo.

Aidha, Mwenyekiti huyo aliwahimiza wazazi kuendelea kuwa na ushirikiano katika kuleta maendeleo ya familia na taifa, huku wakizingatia maadili ya kitaifa na kukumbatia mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yanayoendelea.

Aliongeza kuwa Jumuiya ya Wazazi itaendelea kutoa elimu kwa wazazi kuhusu wajibu wao katika kuleta mabadiliko chanya kwa watoto na jamii kwa ujumla.

Wakati huohuo, Viongozi walisisitiza umoja na mshikamano wa wazazi,huku wakielezea furaha yao ya kuwa sehemu ya familia kubwa ya CCM ambapo Katika tukio hilo,Mgeni rasmi alikata Keki kama ishara ya Upendo kwa wanajumuiya hiyo

Maadhimisho ya Siku ya Wazazi yanakuja ikiwa ni sehemu ya juhudi za Jumuiya ya Wazazi ya CCM kuhimiza ushirikiano na kuendelea kuchangia katika maendeleo ya taifa la Tanzania.

Pamoja na mambo mengine Mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo Comrade Charles Kazungu Mabeyo ambaye pia ni mjumbe wa baraza la Wazazi Taifa kutoka Mkoa wa Geita na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita aliongoza zoezi la kuchangia Damu kwa ajili ya wagonjwa wahitaji wa huduma hiyo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya zoezi la upimaji Afya katika Maadhimisho ya Wiki ya Wazazi Wilaya ya Mbogwe,Mganga Mfawidhi Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe Dr Lubinza Maziku Messu amewashukuru wajumbe wa Jumuiya hiyo kwa kuchangia damu huku akiwaomba kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi la uchangiaji wa Damu maana ni sehemu muhimu ya upendo kwa kuwa kufanya hivyo ni kuokoa maisha ya watu wengine anasema Dr Lubinza.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Mh Sakina Mohamed alisema Wilaya ya Mbogwe iko shwari, Viongozi wanashirikiana katika kutatua changamoto.

Mkuu huyo wa Wilaya amempongeza Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Mbogwe Mathias Nyololo kwa usimamizi mzuri wa Ilani ya CCM na kuwataka wana CCM kuachana na Propaganda zinazofanywa na Wapinzani kwamba CCM haijafanya kitu.

Mkuu wa Wilaya amesema Rais Dkt Samia ameleta zaidi ya Sh bil 70 kwa ajili ya Utekelezaji wa Miradi mbalimbali ikiwemo Miundombinu ya Barabara,ujenzi wa Vituo vya Afya Pamoja na Miradi ya Maji katika Wilaya ya Mbogwe.

Hata hivyo baada ya shughuli ya kuchangia Damu,Mgeni rasmi aliendesha Harambee ya kuchangia fedha kwa ajili ya Ujenzi wa Nyumba ya Katibu wa Jumuiya ya wazazi Wilaya ya Mbogwe ambapo Mgeni alinunua Mabati yenye thamani ya Sh Mil 3,060,000,huku mbao kwa ajili ya kupaua na kumalizia mapambo zikitolewa na Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa mwakilishi wa Mkoa wa Geita Ndugu Evarist Paschal Gervas aliyechangia zaidi ya Sh Mil 4.

Aidha Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mh Khalima Chembemoyo alitambua wadau waliofanikisha Sherehe hiyo kuwa ni Pamoja na Ndugu Evarist Paschal Gervas MNEC kuwakilisha Mkoa Geita,Chacha Wambura (WAJA)ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa Viti Ishirini Bara,Mkurugenzi wa Loeni Schools Elias Ndibato,na Mbunge wa Jimbo la Mbogwe Nicodemus maganga ambaye alichangia Sh 350,000.

MWISHO.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post