NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
AFISA Programu Mkuu kutoka Asasi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na Mazingira na afya ya binadamu- AGENDA, Silvan Mng’anya amesema madini ya risasi yanayopatikana kwenye betri na vifaa vya kielektroniki vina athari kubwa kwa afya ya binadamu, ikiwemo kuathiri mfumo wa damu, uwezo wa kukumbuka, na mfumo wa fahamu.
Ameyasema hayo leo Aprili 10, 2025 Jijini Dar es Salaam wakati wa warsha kuhusu mwelekeo wa urejelezwaji wa betri chakavu iliyoandaliwa na AGENDA kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira -NEMC, na imewakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya mazingira na urejelezwaji wa taka ngumu kama betri za magari na zile zinazotumika kwenye mifumo ya mawasiliano.
Aidha amewataka wenye viwanda vya urejelezwaji wa betri chakavu kuzingatia miongozo iliyowekwa katika ngazi za kimataifa na vilevile wawe tayari kupokea maelekezo ambayo watapewa na wasimamizi wa mazingira hasa pale wanapotakiwa kurekebisha mifumo yao ya urejelezaji.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mapitio ya Tathimini ya Athari kwa Mazingira na Jamii kutoka NEMC Mhandisi Luhuvilo Mwamila alisema kuna haja ya kuwa na muongozo wa pamoja utakaowezesha kutumiwa katika kudhibiti taka za betri chakavu ambazo ziko kwa wingi mtaani.
“Hakuna miongozo rasmi ambayo ipo katika miradi hii lakini kwa sasa iko miongozo ambayo inazungumzia kwa ujumla wake , hivyo tunahitaji miongozo maalumu itakayotumika kudhibiti taka zinazotaka na betri zenye asidi ya risasi". Alisema
Alisema siku za karibuni nchi za Afrika walikuwa na mkutano wa kikanda wapamoja nan chi hizo zimepata nafasi ya kuelezea jinsi ambavyo hali ya viwanda vya aina hiyo ilivyo katika nchi zao na imeonekana kote zinafanana.
“Kwenye mkutano ule tumeona tukae pamoja na kutengeza miongozo ya aina moja itakayosimamia wawekezaji wa viwanda vya kuchakata betri chakavu ambao wengi wanatoka nchi nyingine , tukiwa na muongozo wa pamoja na tukaweka viwango basi itawezesha wawekezaji hao katika nchi yoyote watakayokwenda kufuata miongozo hiyo.” Alieleza
Vilevile Mwanasheria kutoka NEMC, Angela Kileo, alisema kuwa bado kuna upungufu mkubwa wa uelewa miongoni mwa wadau kuhusu sheria zinazohusu usimamizi wa betri chakavu, jambo linalochangia kuwepo kwa uchafuzi wa mazingira huku akibainisha kwamba Serikali za Mitaa zina wajibu wa kudhibiti athari zinazotokana na utupaji holela wa betri hizo.
"NEMC tunazo sheria mama ya mazingira na ziko wazi na zimeelezea vizuri kwamfano mtu anayeshughulika na taka hatarishi kanuni inaeleza anayeharibu mazingira anapaswa alipie. Sheria inaeleza namna gani ya kuomba kibali kama cha chini ya tani tano , uwe na leseni pamoja na TIN". Alisema Kileo.
Pamoja na hayo alisema matumizi ya betri yamekuwa makubwa hivyo betri chakavu zimekuwa nyingi mtaani tunaomba hizo taka watumie kama fursa lakini katika namna ambayo mazingira yetu yatalindwa na afya zetu zitabaki salama.
Naye Mratibu wa Shughuli za Taasisi ya Waendesha Urejeleaji Taka Tanzania-TARA Henry Kazula, alisema kuwa kuwepo kwa sera madhubuti na utekelezaji wake kwa vitendo kutaiwezesha nchi kuwa katika mazingira salama na kulinda afya za wananchi wake.
Post a Comment