Mbunge Esther Malleko atekeleza ahadi yake,akabidhi Mashine za kutotolesha vifaranga vya kuku UWT Mkoa wa Kilimanjaro.
Na Mwandishi wetu.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kilimanjaro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Esther Malleko, ametimiza ahadi yake kwa wanawake wa mkoa huo, kwakuwakabidhi mashine 169 za kutotolesha vifaranga vya kuku (incubators) kwa kata 169 za Mkoa wa Kilimanjaro, zenye thamani ya Shilingi milioni 84.5.
Hafla ya kukabidhi mashine hizo imefanyika jana aprili 13,2025, ambapo pia ameahidi kuwapatia mitaji ya Mayai kwaajili ya kuanza mradi huo,pamoja na kuwapelekea watalamu kwenye kata ili kuwafundisha matumizi sahihi ya mashine hizo pamoja na ufugaji bora wa kuku na utunzaji wa fedha ili kuhakikisha mradi huo unaleta tija.
Amesema ametoa mashine hizo, ambapo ni sehemu ya hadi aliyotoa kwa lengo la kukuza uchumi wa wanawake kwenye kata na matawi ,kwa lengo la kukuza uchumi,lishe pamoja na kuwaunganisha wanawake wote kwenye kata na hata kuondokana na mikopo ya kausha damu ambayo imekuwa ni chanzo cha migogoro kwenye familia nyingi na kuwà rudisha nyuma wanawake wengi kimaendeleo.
"Wanawake wa Kilimanjaro mlinikopesha imani ninawalipa imani, leo nimekuja kutekeleza ahadi kwa kuwakabidhi rasmi mashine hizi (Incubators) ambazo mtazitumia kupitia vikundi vyenu na kunyanyuka kiuchumi," amesema Malleko. "Incubator hizi 169 zimegharamu kiasi cha sh.milioni 84.5,"amesema Malleko.
Aidha, amepongeza Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan,kwa kuupatia Mkoa wa Kilimanjaro trilioni 1.2 katika kipindi chake cha uongozi, amewatua wanawake ndoo kichwani kwa mradi mkubwa wa maji Same Mwanga Kilimanjaro,amejenga hospitali,vituo vya afya na zahanati,amejenga madarasa,barabara na kuboresha utalii katika kipindi chake cha miaka minne katika mkoa huo.
"Sisi Wanawake wa Kilimanjaro hatuna deni na Rais Dk.Samia Suluhu Hassani,tunaahidi kumpigia kura nyingi apate ushindi wa kishindo kwenye uchaguzi 2025," amesema Malleko.
Naye Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa wa Kilimanjaro Ndg.Mercy Mollel, amepongeza Mbunge huyo kwa kutekeleza ahadi yake kwa wanawake wa Mkoa wa Kilimanjaro, na kuwasihi kwamba Mashine hizo wazitunze ili ziwanufaishe kuwakwamua kiuchumi wapate nguvu na hamasa ya kwenda kuzitafuta kura za CCM.
Na baadhi ya wanawake hao, wamempongeza Mbunge huyo kwa kutekeleza ahadi yake, na kwamba mashine hizo sasa zinakwenda kuwainua kiuchumi,kujenga afya ya familia na kuwaunganisha wanawake. Mwisho.
Post a Comment