MISA Tanzania inapenda kuwataarifu wanahabari na umma kwa ujumla kuwa itashiriki kikamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani ngazi ya kitaifa, yatakayofanyika kuanzia tarehe 27 hadi 30 April. 2025, jijini Arusha.
Maadhimisho haya ni jukwaa muhimu la kuwakumbuka na kuwaenzi waandishi wa habari waliopoteza maisha yao wakiwa kazini, kutathmini hali ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, na kujadili mbinu bora za kuimarisha mazingira ya uhuru wa uandishi wa habari nchini na duniani kwa ujumla.
MISA Tanzania itawakilishwa na jumla ya wanachama 20 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania, ambao watashiriki kwenye mijadala, warsha na matukio mbalimbali yanayolenga kuimarisha taaluma ya habari na kutetea haki ya kupata na kutoa taarifa.
Katika maadhimisho haya ya kitaifa, Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MISA Tanzania inawatakia heri na mafanikio wanahabari wote nchini katika kuelekea maadhimisho haya muhimu ya uhuru wa vyombo vya habari duniani. Tunaamini kuwa kupitia ushiriki na mijadala ya pamoja, tutajenga msingi imara wa uhuru, usalama na ustawi wa tasnia ya habari nchini Tanzania. kauli Mbiu ni uhabarishaji kwenye Dunia Mpya: Mchango wa akili Unde kwenye uhuru wa Vyombo vya habari
Imetolewa na:
Bodi ya MISA Tanzania
Tarehe: 26 Aprili, 2025
Post a Comment