
Na Silivia Amandius,
Kyerwa, Kagera
Timu ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia imefanikiwa kuwapatanisha wanandoa wawili waliokuwa katika mgogoro wa mirathi kwa zaidi ya miaka miwili katika Kata ya Kitwechenkura, Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, mkoani Kagera.
Wanandoa hao, Bi. Levina Valentin Tegamaisho na Bw. Johas Josia Bamuhiga, walikua na mvutano tangu mwaka 2022 kuhusu umiliki wa shamba ambalo awali Bw. Johas alikabidhi kwa Bi. Levina kama zawadi. Baadaye, Bw. Johas alitaka kuuza shamba hilo, jambo lililosababisha kutokuelewana baina yao.
Bi. Levina ameeleza kuwa mbali na mgogoro huo wa mali, alikumbana na tukio la kuchomewa nyumba akiwa amelala na binti yake, tukio lililomletea changamoto kubwa ya kukosa mahali pa kuishi. Aliongeza kuwa alihusishwa na masuala ya ushirikina kutokana na hali hiyo, ingawa kesi hiyo bado haijapatiwa ufumbuzi hadi sasa. Hata hivyo, kupitia msaada wa kisheria, anaamini kwamba haki itatendeka.
Katika juhudi za upatanisho, Mratibu wa Timu ya Msaada wa Kisheria, Bi. Kasilida Chimagi, aliwaelimisha wanandoa hao kuhusu umiliki wa mali ndani ya ndoa. Alifafanua kuwa wanandoa wana haki ya kushirikiana katika maamuzi ya kugawa au kuuza mali, na watoto wanapewa urithi kama zawadi, si kama warithi wa moja kwa moja kabla ya kufikia umri unaotakiwa.
Bi. Kasilida alisisitiza umuhimu wa kusameheana na kufuta chuki ili kuendeleza amani na kulea watoto katika mazingira bora, hasa kwa kuwa wanandoa hao wana watoto watatu.
“Nawapongeza kwa kukubaliana kupatana. Ni hatua muhimu kwa ustawi wa familia na watoto. Wanandoa wote wana haki ya kushirikiana katika maamuzi ya mali, hata kama mwanaume amezaa nje ya ndoa,” alisema Bi. Kasilida.
Wanandoa hao wameeleza kuwa msaada huu wa kisheria umeleta mabadiliko chanya kwao na kwa wanajamii wengine, kwani wengi hukosa haki zao kutokana na kutokujua sheria.
Katibu tawala wa halmashauri ya wilaya ya kyerwa Mussa Wazri Gumbo aliyeshiriki katika kikao cha awali cha upatanisho, aliwahimiza wanandoa hao kuishi kwa kuelewana. Alikumbusha kuwa ndoa ni ya watu wawili na watoto ni zawadi kutoka kwa Mungu, hivyo familia inapaswa kuishi kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi.
Alisisitiza pia kuwa migawanyiko ndani ya familia huwadhuru zaidi watoto, ambao huishia kuishi maisha magumu.


Post a Comment