Na Mapuli Kitina Misalaba
Imeelezwa kuwa, Mwanafunzi wa darasa la nne katika
Shule ya Msingi Msufini, anayefahamika kwa jina la Sabina Thadeo mwenye umri wa Miaka 11, amefariki dunia mara
baada ya kugongwa na pikipiki katika barabara ya kutoka mjini Shinyanga kuelekea Mwawaza,
eneo la Mtaa wa Masekelo, Manispaa ya Shinyanga.
Tukio hilo limetokea Aprili 3, 2025 majira ya saa kumi na moja
jioni wakati wanafunzi walipokuwa wakielekea nyumbani kutoka shuleni, ambapo
bodaboda mmoja anadaiwa kuendesha kwa mwendo kasi na kumgonga mwanafunzi huyo ambaye
aliyekuwa akivuka barabara.
Akizungumza na Misalaba
Media, Mwenyekiti wa Mtaa wa Masekelo, Elias Mg’waya, amethibitisha
kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa mwendesha bodaboda huyo alikamatwa na
wananchi wenye hasira ambao walimfikisha katika ofisi ya serikali ya mtaa kwa
hatua zaidi.
“Kuna barabara yetu kubwa ya kutoka mjini
Shinyanga kuelekea Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Mwawaza ilikuwa
majira ya saa kumi na moja wanafunzi walikuwa wanakatisha kwenda nyumbani,
lakini wakati wakivuka mwanafunzi mmoja wa darasa la nne mwenye umri wa Miaka
11 aligongwa na pikipiki ambaye ni mwendesha bodaboda alikuwa anaendesha kwa
mwendo kasi, baada ya kumgonga mtoto huyo alifariki dunia palepale,”
amesema Mg’waya.
Amesema baada ya tukio hilo walijaribu kuwasiliana
na polisi kwa ajili ya msaada wa haraka, lakini hawakupata majibu kwa wakati,
hali iliyowalazimu wananchi kuisimamisha gari ya wagonjwa iliyokuwa inapita na
kuomba msaada wa kuusafirisha mwili wa marehemu hadi mochwari.
“Wananchi walifanikiwa kumkamata
bodaboda huyo wakamleta ofisi ya serikali ya mtaa wa Masekelo, baada ya kufika
ofisini kwangu nikawapigia polisi lakini sikupata msaada kwa uharaka, bahati
nzuri ilipita gari ya ambulance wananchi wakasimama barabara gari hiyo
ikasimama ndiyo tukapata msaada ya kuubeba mwili ukapelekwa mochwari, lakini
pia nilipata msaada wa yule mtuhumiwa akapelekwa kituo cha polisi moja kwa
moja,” amesema Mg’waya.
Aidha, Mg’waya amesema ajali hiyo si ya kwanza
kutokea katika eneo hilo, na kwamba hali hiyo inachangiwa na ubovu wa barabara
ambao umekuwa ukihatarisha maisha ya watumiaji, hasa watoto na watembea kwa
miguu.
“Ajali hiyo pia imechangiwa na ubovu wa
barabara, kumekuwa na ajali za mara kwa mara ambazo zinasababishwa na ubovu wa
barabara. Mimi niiombe serikali kama hakuna bajeti ya kuiboresha barabara hiyo
kwa kiwango cha lami basi watuwekee hata bamzi ili watumiaji wa vyombo vya moto
hasa bodaboda wasiwe wanapita kwa kasi,” ameongeza.
Misalaba Media inaendelea kuwasiliana na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ili kufahamu hatua zaidi zilizochukuliwa dhidi ya mtuhumiwa huyo.
Mpaka sasa mwili wa marehemu upo mochwari katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga
Post a Comment