" NYANZA WAANZISHA MKAKATI WA KUINUA ZAO LA KAHAWA BUCHOSA

NYANZA WAANZISHA MKAKATI WA KUINUA ZAO LA KAHAWA BUCHOSA


Na Tonny Alphonce,Mwanza

Chama Kikuu  cha Ushirika Nyanza kimeanza rasimi kuwekeza nguvu  katika zao la Kahawa  kwa lengo  la kuongeza uzalishaji  na kuwainua wakulima  wa  Halmashauri ya Buchosa Mkoani Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari  Mwenyekiti wa Bodi ya Chama  kikuu cha Ushirika cha Nyanza  Bw. Leonard Lyabauma  amesema Nyanza itashirikiana na serikali katika kutatua changamoto walizonazo wakulima wa Kahawa  kwa kutafuta ufumbuzi wa upatikanaji wa  mbegu,madawa pamoja na masoko.

Akizungumzia sababu za chama cha Nyanza kuingia kwenye zao la Kahawa ,Lyabalima amesema ni kutokana na kushuka kwa uzalishaji wa Pamba katika wilaya ya Buchosa na baadhi ya wakulima na wanachama wa Nyanza kuanza kulima Kahawa.

“Lengo letu sasa Nyanza tunajipanga kukutana na wakulima na wanachama wetu wote wanaolima zao hili la Kahawa ili tuweze kuwasaidia waweze kuongeza uzalishaji lakini pia kupata uhakika wa mbegu madawa pamoja na kuwatafutia soko la uhakika”alisema Lyabalima

Meneja wa kanda ya Buchosa Bw. Kalunga Ibrahimu amesema maamuzi ya chama kikuu cha Ushirika Nyanza kuingia katika zao la Kahawa yamepokelewa vizuri na wakulima wakiwa na matumaini makubwa ya kukufuka kwa zao hilo ambalo lilikosa usimamizi.
Nae afisa kilimo wa halmashauri ya wilaya ya Buchosa Nestory Mjojo amesema programu hii ya kuwahamasisha wakulima wa Kahawa  kuongeza uzalishaji wa zao hilo utasaidia kuwashawishi wakulima wengi kurudi kuwekeza tena kwenye zao hilo.

Akizungumzia kuhusiana na changamoto wanazokutananazo wakulima hao wa  Kahawa  Mojojo amesema kitu chakwanza  watakachofanya ni kuwatambua wakulima hao na kisha kuhakikisha wote wanaingia katika ushirika ambao tayari upo ili iwe rahisi kwao kupewa huduma.

“kwa sasa katika wilaya yetu ya Buchosa tunazalisha tani 30 lakini tunauhakika tukienda pamoja tunaweza kuzalisha hadi tani 50 na kuendelea ambapo lengo ni kufikia tani 200 ili kwamba tuwe na minada ambayo itakuwa inafanyikia hapa hapa Buchosa na kuachana na walanguzi ambao wanawanyonya wakulima”alisema Mjojo
Mkulima Jonathan Misogi wa kijiji cha Lumea anasema changamoto kubwa waliyonayo katika zao hilo la Kahawa na upatikanaji wa Miche pamoja na soko la uhakika
Misogi amesema mwanzoni TAKRI na Halmashauri waliwasaidia kupata Miche lakini baadae walijitoa na hapo ndipo tatizo la upatikanaji wa Miche ya kahawa ulipoanzia.

Kwa upande wake Seleman Ndaki  mkulima wa Kahawa anasema changamoto anayokutananayo ni mbolea pamoja na wadudu wanaoshambulia miti ya Kahawa ambapo hadi sasa hajajua dawa ambayo inaweza kupambana na wadudu hao.

Kwa juhudi zinazoendelea kuwekwa na Chama Kikuu Cha Ushirika Nyanza  pamoja na ushirikiano wa Serikali na Wakulima ,matumaini ya kufufua  na kuendeleza zao la Kahawa katika wilaya ya Buchosa yanaonekana  kuimarika.
 


Post a Comment

Previous Post Next Post