Mwanamuziki mahiri wa taarab nchini Tanzania, Khadija
Omary Abdallah Kopa, pamoja na Pastor Dr. Rose Shaboka, wametua rasmi mjini
Kahama kwa ajili ya kushiriki kwenye Tamasha la Mwanamke Chuma 2025,
linalotarajiwa kufanyika kesho tarehe 12 Aprili katika ukumbi wa Malex Hall.
Khadija Kopa pamoja na Dr. Rose wameshiriki kipindi maalum kupitia Gold FM, wakitumia
fursa hiyo kuzungumza na wananchi wa Kanda ya Ziwa na Watanzania kwa ujumla,
wakiwahamasisha kujitokeza kwa wingi kwenye tamasha hilo linalolenga kumwinua
mwanamke katika nyanja mbalimbali za maisha.
Khadija Kopa, anayefahamika kwa sauti yake ya kuvutia
na ujumbe mzito wa nyimbo zake, amesema amefurahishwa na tamasha hilo ambapo
amewahimiza wakazi wa kanda ya ziwa kujitokeza kwa wingi ili kushuhudia burudani ya nyimbo zenye ujumbe.
Kwa upande wake, Dr. Rose Shaboka amesisitiza
umuhimu wa mwanamke kupewa nafasi sawa katika uongozi, uchumi, elimu na masuala
ya kiroho huku akieleza kuwa tamasha hilo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha
wanawake wa rika na taaluma mbalimbali ili kupeana maarifa na kuhamasishana.
Tamasha la Mwanamke Chuma mwaka huu linatarajiwa kuwa kubwa zaidi, likihusisha utoaji wa tuzo kwa wanawake waliotoa mchango mkubwa katika jamii kupitia uongozi, ujasiriamali, elimu, afya na harakati za kijamii.
Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana wa CCM (UVCCM), Jokate Mwegelo, huku wageni wengine wa serikali na taasisi binafsi pia wakitarajiwa kuhudhuria.
MISALABA MEDIA tunatarajia kurusha mubashara tamasha
hili kupitia channel ya YouTube, kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya
kushuhudia tukio hilo muhimu la kumwinua mwanamke wa Kitanzania.

Post a Comment