
Mkuu wa mkoa wa Dar es Saalam Albert Chalamila,akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo Pichani) jijini Dodoma.
……..
SAA chache baada ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Heche na wafuasi wake kukamatwa na Jeshi la Polisi maeneo ya Kariakoo wakifanya mkutano wa hadhara.
Mkuu wa mkoa wa Dar es Saalam Albert Chalamila, ametoka mbele ya vyombo vya habari na kusema kuwa anaunga mkono kilichofanywa na jeshi la polisi na kudai kuwa hawawezi kuruhusu mizaa iendelee kwa kila mtu kutaka kufanya mikutano sehemu nyeti kama hizo anavyotaka yeye.
Amesema Heche amekamatwa kutokana na kuendesha mkutano katika eneo lisiloruhusiwa kisheria.
“Hatuwezi kuendelea kuruhusu mizaha kama hii iendele kwani eneo la Kariakoo ni eneo nyeti sana kuna watu wanafanya biashara zao kutoka nje na ndani ya nchi kama tutaendelea kuruhusu kila mahali kuwa eneo la siasa basi ipo siku watu watataka kufanya mikutano ya hadhara kwenye makanisa, misikiti, hospitali na maeneo mengine ambayo hayajaruhusiwa,”amesema Chalamila
Aidha, ameagiza Jeshi la polisi kwa kiongozi yeyote ambaye atabainika kukaidi amri hiyo kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Chalamila amesema ni muhimu wanasiasa kuheshimu taratibu za kufanya mikutano ya hadhara na kwamba sheria itachukua mkondo wake kwa yeyote atakayekiuka.
Aidha, Chalamila amezungumzia tetesi za kuwapo kwa kundi la watu wanaopanga kufanya maandamano tarehe 24 mwezi huu, akisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha amani inadumishwa. Ametoa wito kwa wananchi kufuata sheria na kuepuka kushiriki katika mikusanyiko isiyo halali.
Serikali imesisitiza kuwa haitafumbia macho vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.
Post a Comment