Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha amezindua rasmi wiki ya maadhimisho kuelekea kilele cha Siku ya Wafanyakazi Duniani Mei 1, 2025, hulu akitoa wito kwa waajiri wote mkoani Shinyanga kuwaruhusu wafanyakazi wao kushiriki kikamilifu kwenye maadhimisho haye.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika katika Uwanja wa Kambarage uliopo Manispaa ya Shinyanga, RC Macha amesema wiki ya wafanyakazi ni fursa ya kipekee kwa wafanyakazi kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii, zikiwemo huduma za afya na elimu, ambazo zimeandaliwa kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi moja kwa moja.
“Waajiri mnapaswa kuelewa kuwa ushiriki wa wafanyakazi katika maadhimisho haya siyo tu ni haki yao, bali ni njia mojawapo ya kuimarisha mshikamano, uhusiano na hivyo kuongeza morali kazini,” alisema RC Macha.
Aidha, RC Macha alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa uhusiano mzuri kati ya waajiri na waajiriwa, akibainisha kuwa ushirikiano huo ni kichocheo kikubwa cha kuongeza tija na ufanisi katika maeneo ya kazi.
Katika hotuba yake, RC Macha alipongeza juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyakazi nchini.
“Rais wetu amekuwa akionesha dhamira ya dhati ya kuwapigania wafanyakazi. Tayari baadhi yao wamelipwa malimbikizo ya mishahara na wengine waliokuwa wamechelewa kupandishwa vyeo tayari wamepandishwa na wanaendelea kupata haki zao stahiki,” aliongeza RC Maxha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Shinyanga, Bw. Yohana Maremi, alisema kabla ya uzinduzi huo wanachama wa TUCTA walijitolea kufanya usafi katika Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga kama sehemu ya kuadhimisha wiki hiyo ya wafanyakazi.
Amesema jitihada hizo zimechangia kuboresha mazingira ya utoaji huduma hospitalini hapo na kuonesha mfano wa uwajibikaji wa kijamii kwa wafanyakazi.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu isemayo: "Uchaguzi Mkuu 2025, Utuletee viongozi wanaojali Haki na Maslahi ya Wafanyakazi, Sote Tushiriki"
Post a Comment