Klabu ya Simba SC imeandika historia nyingine kubwa katika soka la Afrika baada ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup), kwa kuiondosha Stellenbosch FC ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 1-0.

Katika mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye Uwanja wa Moses Mabhida jijini Durban, timu hizo zilitoka sare ya bila mabao (0-0), matokeo yaliyoiwezesha Simba kusonga mbele kwa faida ya ushindi wa goli moja walioupata kwenye mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam.

Hii ni mara ya pili Simba kufika hatua ya fainali ya michuano ya CAF, baada ya mara ya kwanza kufanya hivyo mwaka 1993. Safari hii, Wekundu wa Msimbazi wanasubiri kumenyana na mshindi kati ya CS Constantine ya Algeria na RS Berkane ya Morocco.

Fainali ya kwanza itapigwa Mei 17, 2025, huku mchezo wa marudiano ukipangwa kuchezwa Mei 25, 2025.

Kombe la Shirikisho Afrika lilianzishwa mwaka 2004 kufuatia kuunganishwa kwa michuano ya African Cup Winners' Cup (iliyodumu kuanzia 1975) na CAF Cup (iliyoanzishwa mwaka 1992).



RAIS SAMIA ATOA PONGEZI KWA KLABU YA SIMBA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameipongeza Klabu ya Simba kwa ushindi wao katika mchezo wa Mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF Confederation Cup) na kuandika historia ya kufuzu kwa fainali ya mashindano hayo.

Kupitia salamu zake, Rais Samia amesema kuwa ushindi huo umeipa Tanzania heshima kubwa katika soka la Afrika, na amewapongeza wachezaji, benchi la ufundi na uongozi wa klabu hiyo kwa juhudi zao kubwa.

"Pongezi za dhati kwa Klabu ya Simba kwa ushindi katika mchezo wa Mashindano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF Confederation Cup), na kuandika historia ya kufika fainali ya mashindano haya. Mmeipa nchi yetu heshima kubwa. Nawatakia kila kheri. Mnayo hamasa yangu wakati wote"

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA