" TAMASHA LA KULIOMBEA TAIFA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU KUFANYIKA JUNI 21 JIJINI DAR

TAMASHA LA KULIOMBEA TAIFA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU KUFANYIKA JUNI 21 JIJINI DAR











Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, jamii ya Watanzania imetakiwa kuungana katika maombi kwa ajili ya amani na ustawi wa taifa kupitia Tamasha la Kitaifa la Maombezi linalotarajiwa kufanyika Juni 21, 2025 jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari Aprili 13, Mkurugenzi wa Msama Promotion na muasisi wa Tamasha hilo, Alex Msama, alisema tamasha hilo litaanzia jijini Dar es Salaam kisha kuzunguka mikoa mingine 25 nchini, likiwa na lengo la kuuombea uchaguzi uwe wa amani na kumpa Mungu nafasi ya kuwaongoza Watanzania kupata viongozi sahihi.

“Tamasha hili ni fursa ya kipekee kwa taifa kuliombea amani, mshikamano na kumpa Mungu nafasi ya kutuongoza katika uchaguzi. Tumeanza maandalizi mapema na tayari waimbaji kutoka Afrika Kusini, Nigeria na Congo wamekubaliana kushiriki, huku mazungumzo yakiendelea na Rwanda,” alisema Msama.

Aidha, alitoa wito kwa wadau na makampuni kujitokeza kudhamini tamasha hilo kutokana na gharama kubwa za kuandaa matukio makubwa ya kiibada yatakayowakutanisha waimbaji wa kimataifa na wa ndani.

Kwa upande wake, Philip Mwotsi, Mchungaji kutoka Kanisa la FPCF alisema maombi haya ni silaha ya taifa kuelekea kipindi kigumu cha uchaguzi. “Kupitia maombi haya, tunaamini Mungu atatupa viongozi walio bora na wenye maono kwa taifa,” alisema.

Naye Mchungaji Rose David kutoka Kanisa la Pentekoste alitoa wito kwa Watanzania kushiriki kwa wingi katika tamasha hilo, akisema: “Katika umoja na maombi, tunaweza kuiweka nchi yetu mikononi mwa Mungu na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.”

Post a Comment

Previous Post Next Post