Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,
Ndg. Kailima, R. K akifafanua jambo.
Na. Mwandishi Wetu Dodoma
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, vyama vya
siasa na Serikali kesho tarehe 12 Aprili, 2025 wanatarajiwa kusaini Kanuni za
Maadili ya Uchaguzi yatakayotumika kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika
Oktoba mwaka huu.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum na vyombo
vya habari mkoani Dodoma leo tarehe 11 Aprili, 2025 Mkurugenzi wa Uchaguzi wa
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndugu. Kailima Ramadhan amesema chama cha siasa
ambacho hakitasaini maadili hayo hakitaruhusiwa kushiriki kwenye uchaguzi huo.
Ndugu. Kailima amesema maadili hayo
yameandaliwa kwa mujibu wa kifungu cha 162 (1), (2) na (3) cha Sheria ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 ambacho kinaitaka Tume
baada ya kushauriana na vyama vyote vya siasa na Serikali, kuandaa na
kuchapisha katika Gazeti la Serikali Kanuni za Maadili ya Uchaguzi
zitakazoainisha maadili ya vyama vya siasa, Serikali na Tume wakati wa kampeni
za uchaguzi na uchaguzi na utaratibu wa utekelezaji wake.
Amesema kifungu hicho kinaelekeza kuwa kanuni
za maadili zitasainiwa na kila chama cha siasa, kila mgombea kabla
hajawasilisha fomu ya uteuzi, Serikali na Tume na zitapaswa kuzingatiwa na
wahusika wote waliosaini.
Ameongeza kuwa tayari maandalizi yote muhimu
yameshafanyika na mawasiliano yameshafanyika baina ya Tume, Serikali na vyama
vya siasa na kwamba kinachosubiriwa ni kuwasili kwa wahusika jijini Dodoma kwa
ajili ya kusaini kanuni hizo za maadili kesho.
Amefafanua kuwa zoezi hilo litafanyika kwa
siku moja tu na kwamba baada ya hapo chama ambacho hakijasaini kanuni hizo za
maadili hakitapata fursa ya kusimamisha wagombea.
Katika hatua nyingine, Kailima amesema Tume
inaendelea vizuri na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kwamba tayari
imekamilisha awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
na kwamba maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwa awamu ya pili yanaendelea
ambapo Tume inatarajiwa kutangaza ratiba ya zoezi hilo hivi karibuni.
Kifungu cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa
Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, ambacho kinaipa Tume jukumu la
kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili, kati ya uchaguzi mkuu
mmoja uliomalizika na siku moja kabla ya uteuzi wa wagombea wa uchaguzi mkuu
unaofuatia.
Tayari Tume imekamilisha awamu ya kwanza ya
uboreshaji wa Daftari ambao ulifanyika nchi nzima kuanzia tarehe 20 Julai, 2024
hadi tarehe 25 Machi, 2025.
Post a Comment