" UZINDUZI WA SHINA LA MAMA SAMIA KATA YA KITANGILI WAANDIKA HISTORIA MPYA

UZINDUZI WA SHINA LA MAMA SAMIA KATA YA KITANGILI WAANDIKA HISTORIA MPYA

Na Daniel Sibu, Misalaba Media

Katika kuendeleza juhudi za kuimarisha uhai wa chama ngazi ya mashina, leo tarehe 17 Aprili 2025, Shina la Mama Samia katika Kata ya Kitangili limezinduliwa rasmi na Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Ndugu Abdulazizi S. Sakala, katika tukio lililohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi, Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), pamoja na wananchi wa Kitangili.

Katika hotuba yake ya uzinduzi, Ndugu Sakala alieleza kuwa Kitangili leo imeandika historia kubwa kwa kuzindua shina hili muhimu, akisema 

“Hii ni historia ya kipekee. Tumeanzisha shina la Mama Samia kama ishara ya kuthamini na kuunga mkono juhudi na mafanikio ya Rais wetu. Sisi vijana wa Shinyanga tupo tayari kuendelea kusimama na CCM, tukisema kwa kauli moja: Mama full box operation!”

Viongozi wa Kata Watia Nguvu

Mwenyekiti wa UVCCM Kata ya Kitangili, Bi. Ester James Zephania, kwa furaha alisisitiza kuwa:

 “Leo ndiyo leo. Hayawi hayawi, hatimaye yamekuwa! Tupo chini ya uongozi bora wa mama yetu, Diwani Mariamu Nyangata, ambaye ametuletea maendeleo halisi: madaraja, miundombinu, na huduma bora. Tunampongeza pia Mbunge wetu Mhe. Patrobas Katambi na Rais wetu Mama Samia kwa kutekeleza ilani kwa vitendo!”

Kwa upande wake, Katibu wa UVCCM Kata ya Kitangili, Bi. Neema Edward Robert, aliwasilisha taarifa ya hali ya chama akibainisha mafanikio yaliyopatikana licha ya changamoto zilizopo kama vile ubovu wa majengo ya shule ya Ihuleng’ula na ukosefu wa soko la biashara.

“Uhai wa jumuiya ni mzuri. Tumefanikiwa kutembelea matawi yote, kuvuna wanachama wapya, na kuwasiliana kwa karibu na makundi ya vijana kama bodaboda na wafyatua tofali. Tunapongeza kazi kubwa inayofanywa na viongozi wetu,” alisema.

Diwani: Bilioni 3 Zimetenda Kazi Kitangili

Diwani wa Kata ya Kitangili, Bi. Mariamu Nyangata, alielezea mafanikio yaliyopatikana tangu mwaka 2020: 

“Tulikinadi chama chetu tukiwa na ilani, leo tumetekeleza takribani yote. Elimu, afya, maji, barabara, umeme – yote haya yamefanyika. Shule ya Ihuleng’ula inakwenda kujengwa upya. Bilioni 3 tayari zimefanya kazi hapa. Hakika kazi imeonekana!”

Nao Madiwani wa viti maalum wakiongozwa na Bi. Moshi Kanji waliongeza kuwa maendeleo yaliyofanyika ni ya kiwango cha juu, ikiwa ni pamoja na kujengwa kwa zahanati na madaraja ambayo sasa yanaunganisha wakazi wa kata hiyo kwa urahisi. 

Msimamo wa Vijana: Tuko Tayari Kutoa Kura kwa CCM

Katika kuhitimisha tukio hilo, Ndugu Sakala alisisitiza kuwa vijana wa UVCCM wako mstari wa mbele kuhakikisha ushindi wa CCM katika uchaguzi ujao kwa ngazi zote: 

“Tumejipanga. Mama tumemteua kwa nafasi ya Urais, sasa ni muda wa kuhakikisha tunaweka madiwani na wabunge wa CCM. Tuchague viongozi wenye dira na kazi kubwa kama ilivyoonekana hapa Kitangili.”

Uzinduzi wa Shina la Mama Samia Kitangili siyo tu tukio la kisiasa, bali ni uthibitisho wa mshikamano, matumaini na maendeleo yanayochochewa na chama tawala kupitia vijana wake. Ni hatua nyingine katika safari ya kuhakikisha kila kijana anashiriki katika ujenzi wa Taifa kwa kauli na matendo. Hakika, Kitangili leo imeandika historia mpya yenye mwelekeo wa matumaini.

 





 

Post a Comment

Previous Post Next Post