" DC MTATIRO ATAKA VIJANA NA WANAWAKE WACHUKUA HATUA KUPINGA UONGOZI KWA NJIA YA RUSHWA KWENYE UCHAGUZI MKUU 2025

DC MTATIRO ATAKA VIJANA NA WANAWAKE WACHUKUA HATUA KUPINGA UONGOZI KWA NJIA YA RUSHWA KWENYE UCHAGUZI MKUU 2025

Na Daniel Sibu, Misalaba Media

Mtandao wa vijana wa Taifa Letu Kesho Yetu Movement (TK Movement) Wilaya ya Shinyanga Mjini umefanya kongamano la aina yake lililobeba mjadala mzito kuhusu nafasi ya vijana na wanawake katika kuzuia upatikanaji wa viongozi kwa njia ya rushwa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025.

Kongamano hilo limeongozwa na mada yenye nguvu isemayo: “Uongozi Bila Rushwa 2025 Ni Wajibu wa Vijana na Wanawake”, likilenga kuleta ukombozi wa kifikra kwa vijana na wanawake ili wasitumiwe na watu wenye nia ovu ya kutaka madaraka kwa njia ya rushwa.

Mgeni rasmi wa kongamano hilo ni mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro, amewahamasisha vijana na wanawake kusimama kidete kupinga matumizi ya fedha kama njia ya kupata uongozi.

“Rushwa si kitu cha mbali, iko kwenye mifumo yetu, kwenye siasa zetu, na mara nyingi tunaiona lakini tunaamua kunyamaza. Vijana na wanawake mnao uwezo mkubwa wa kuikataa, kuifichua na kuizima kabla haijawa sumu kwa taifa letu,” alisema kwa msisitizo mkubwa.

Amewataka vijana kuchagua viongozi kwa misingi ya uadilifu, uwezo, na dira ya kweli ya maendeleo – si kwa vichwa vya khanga, pesa, wala ahadi hewa.

Mwakilishi kutoka TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga, Bw. Mhamedi Doo, amewapa washiriki elimu kuhusu aina mbalimbali za rushwa na athari zake kwa jamii. Alieleza kwamba rushwa inapotumika kupata uongozi, matokeo yake ni kutokuwajibika, ukosefu wa huduma bora, na maamuzi yasiyo na maslahi ya wananchi.

Bi. Felista Buzuka, mlezi wa TK Movement, alisisitiza umuhimu wa vijana kutumia sauti zao kwa njia sahihi.

“Msitumike, msinunuliwe, na msikubali tamaa ififie ndoto zenu. Taifa linaangalia nyie kulinda misingi ya haki,” alisema kwa msisitizo.

Kwa mujibu wa waandaaji wa kongamano hilo, TK Movement inalenga kuandaa kizazi cha vijana na wanawake watakaokataa kutumika kama chombo cha kuhujumu mustakabali wa taifa kupitia rushwa.

“Tunataka vijana na wanawake wasiwe madaraja ya wanasiasa wenye nia ovu. Tunahitaji viongozi wanaotokana na maono, si kwa hongo,” alisema Mratibu wa TK Movement Wilaya ya Shinyanga Mjini, Moses Mshadatila.

Kongamano hili limeibua msukumo mpya kwa vijana na wanawake katika Wilaya ya Shinyanga Mjini kuchukua nafasi ya kuwa walinzi wa haki na maadili ya uchaguzi. Kwa ukombozi wa kifikra unaoendelea kuenezwa na TK Movement, matumaini ni makubwa kuwa mwaka 2025 utazaliwa uongozi unaotokana na uadilifu – si hongo.


Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro akizungumza kwenye kongamano hilo leo Aprili 5, 2025











































 

Post a Comment

Previous Post Next Post