" VIPAUMBELE 14 VYA TAMISEMI HIVI HAPA - MHE MCHENGERWA

VIPAUMBELE 14 VYA TAMISEMI HIVI HAPA - MHE MCHENGERWA

 


OR TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Wizara yake imepanga kutekeleza vipaumbele 14 katika mpango wa bajeti wa mwaka 2025/26.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara na taasisi zake kwa mwaka 2025/26, Mhe. Mchengerwa amesema utekelezaji wa mpango wa majeti unazingatia vipaumbele vya kusimamia shughuli za utawala bora, kukuza demokrasia, ushirikishwaji wa wananchi na Ugatuaji wa Madaraka kwa Umma (D by D).

Pia kuratibu na kusimamia utekelezaji wa shughuli za utoaji wa huduma za jamii, kuratibu na kusimamia mkakati wa kuongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti matumizi yasiyo na tija katika ngazi zote na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mikoa, mamlaka za serikali za mitaa na taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Mchengerwa amesema kufanya uratibu wa usimamizi wa mifumo ya TEHAMA, kuendeleza rasilimali watu katika ngazi zote za Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kuratibu na kusimamia shughuli za kuboresha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, mikoa na mamlaka za serikali za mitaa na kuratibu na kushiriki michezo ya shule za msingi (UMITASHUMTA), sekondari (UMISSETA) na mashindano ya michezo ya shule za sekondari za Afrika Mashariki.
Amesema pia kuratibu shughuli za utendaji wa kazi wa taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kuratibu na kusimamia ujenzi wa miradi ya maendeleo katika ngazi zote za Ofisi ya Rais-TAMISEMI, kuratibu uibuaji wa miradi ya kimkakati na miradi inayopaswa kutekelezwa kwa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika mamlaka za serikali za mitaa na kusimamia na kuratibu shughuli za utunzaji wa mazingira na uhifadhi wa maliasili katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa.

Kipaombele kingine ni kuratibu na kusimamia utekelezaji wa afua za mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na uendelezaji wa utalii, uhamasishaji wa nishati safi ya kupikia na uendelezaji wa biashara ya kaboni katika mikoa na mamlaka za serikali za mitaa na kuratibu shughuli za uendelezaji wa vijiji na miji kwenye mamlaka za serikali za mitaa.

Post a Comment

Previous Post Next Post