Waandishi wa habari kutoka Manispaa ya Shinyanga kupitia Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga Press Club – SPC), wametembelea bustani ya wanyama ya Jambo Zoo iliyopo eneo la Ibadakuli, Mjini Shinyanga, inayomilikiwa na Kampuni ya Jambo Group.
Ziara hiyo imefanyika leo ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha utalii wa ndani pamoja na kuwaunga mkono wawekezaji wazawa, ambapo imeratibiwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na kampuni hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mhifadhi wa Jambo Zoo, Babuu Burhan Kajuna, amesema bustani hiyo imebeba uzito mkubwa wa kielimu na kiburudani kwa jamii kutokana na uwepo wa wanyama wa aina mbalimbali waliopatiwa mafunzo maalum na kuzoea mazingira ya kibinadamu.
“Tunawashukuru waandishi wa habari kwa kutembelea Jambo Zoo. Tunawakaribisha wananchi wote waje kufanya utalii wa ndani hapa Shinyanga. Bei zetu ni rafiki kabisa – watu wazima ni shilingi 20,000 na watoto ni shilingi 10,000,” amesema Kajuna.
Ameongeza kuwa wageni wanaofika katika bustani hiyo hupata nafasi ya kujifunza tabia za wanyama, kupiga nao picha kwa ukaribu pamoja na kuwalisha chakula kwa mikono yao, jambo ambalo huongeza hamasa kwa watoto na familia kwa ujumla.
Kwa upande wake, Msimamizi wa Chapa kutoka Jambo Group, Nickson George, amewataka wakazi wa Shinyanga na mikoa jirani kuitumia vema fursa ya sikukuu ya Pasaka kwa kutembelea bustani hiyo wakiwa na familia zao, huku wakifurahia vinywaji vipya vya kampuni hiyo vya Jambo Lemon Lime na Jambo Power Boom.
Naye Mratibu wa ziara hiyo, Marco Maduhu, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Tendaji ya SPC, ameipongeza Kampuni ya Jambo Group kwa uwekezaji wa bustani hiyo, akisema umeendelea kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, katika kuhamasisha utalii kupitia filamu ya The Royal Tour.
Bustani ya Jambo Zoo imekuwa kivutio muhimu kwa wakazi wa Shinyanga na wageni, ikiwa sehemu ya utalii wa elimu, burudani na uhifadhi wa wanyama katika mazingira rafiki kwa familia na watoto.

Post a Comment