" Wanachuo wa IAA wakumbushwa kuifahamu historia ya Muungano wa Tanzania.

Wanachuo wa IAA wakumbushwa kuifahamu historia ya Muungano wa Tanzania.

  


Katika uzinduzi wa kongamano la miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lililofanyika katika Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Wanachuo wamekumbushwa kuifahamu historia ya muungano huo ili kuulinda na kuudumisha kwa maslahi mapana ya vizazi vijavyo.

Amezungumza hayo wakati akifungua kongamano hilo Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Islam Seif Salum, na kufafanua kuwa Muungano ulitokea kwa maridhiano ya Waasisi  Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Amani Abeid Karume kwa kuzingatia maoni ya Wananchi.

Aidha amesisitiza wananchi kutanguliza utambulisho wao (Utanzania) kama ambavyo watu wa taifa la Marekani wanafanya siku zote, hii yote ikidhihirisha kuwa Muungano ni tunu inayotakiwa kulindwa na kila mmoja.

"Sote tunafahamu, kuwa na sarafu moja na katiba moja si jambo la kawaida, na hakuna muungano wowote usiokuwa na changamoto ingawa kwa upande wetu changamoto ni chache na zinaendelea kufanyiwa kazi.

Pia amesisitiza elimu ya muungano kutolewa shuleni kuanzia ngazi ya msingi hadi elimu ya juu ili kueneza ufahamu wa nini maana ya muungano, sifa za muungano na kwanini unatakiwa kulindwa na kudumishwa, "Wakati muungano unafanyika idadi ya watu ilikuwa takriban milioni 9 na leo idadi imefikia milioni 60, wamebaki watu wachache walioshuhudia muungano huu, ambapo kwa upande wa Zanzibar  wamebaki takribani watu 92,000, sasa ni  wakati sahihi wa kila mmoja kuufahamu muungano vizuri na kutathmini faida zake badala  ya kuuponda" ameeleza Dkt.Islam.

Sambamba na hayo ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha Uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha unatimiza lengo lake la kujenga chuo cha Uhasibu kwa upande wa Zanzibar, hatua hiyo itaongeza ushirikiano, kuimarisha muungano na kukuza uchumi kwa pamoja.

Awali akieleza katika muktadha wa muungano, Prof. Eliamani Sedoyeka Mkuu wa Chuo -IAA, amesema chuo kimekuwa na mahusiano mazuri na Zanzibar ambapo zaidi ya wanafunzi 100 hujiunga na chuo kwa mwaka, nakueleza dhamira ya IAA kufungua Kampasi visiwani Zanzibar ili kufundisha fani zitakazoendana na mabadiliko makubwa yaliyopo.

Amesema katika  mipango iliyopo ya kujitanua, wanalenga kufikia hatua ya kufungua vyuo vya uhasibu na kozi nyingine Kitaifa, Kikanda na Kimataifa, pia ameelezea mkakati wa kujipatia kipato nje na ada, amesema wamejenga  mabweni, wanatarajia kufungua kituo cha redio na televisheni hatua itakayowapunguzia wananfunzi mzigo wa ada na kukuza uchumi wa taasisi hiyo.

"Kila mwaka mwaka tumekuwa tukipata wanafunzi wanaomaliza masomo yao hapa kutoka visiwa vya Zanzibar, hii imetusukuma zaidi kufikiria  kufungua kampasi ya chuo visiwani humo ili pia kukuza uchumi kupitia utalii" amesema Prof. Sedoyeka.

Katika namna hiyohiyo  Mhadhiri mwandamizi wa IAA Dkt. Hellen Meshack ambaye wazazi wake ni mazao ya muungano kutoka bara na visiwani amesema muungano una faida nyingi ikiwemo  mashirikiano ya vyakula, ajira na masumala ya mila na desturi.

"Kwa upande wangu Muungano ni mzuri mno na una faida nyingi, kwa mfano Zanzibar kuna hoteli nyingi lakini wakazi wake hawapendi kazi hiyo, hivyo wanategemea wafanyakazi kutoka bara, hii inaonyesha umuhimu na faida ilivyo kubwa" amesema Dkt. Hellen.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Vijana wa chuo cha uhasibu Arusha Davis Chami ameeleza namna atakavyoendelea kuhubiri injili kwa wanafunzi wote, na kuhakikisha wanaulinda muungano bila kuwepo yeyote wa kuuvunja.






Post a Comment

Previous Post Next Post