" WANNE WASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA UNYANG’ANYI WA KUTUMIA SILAHA

WANNE WASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA UNYANG’ANYI WA KUTUMIA SILAHA






Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa wanne, Salim Boniface @ Msambule [36] Mkazi wa Ihowanza Malangali – Mufindi, Charles Lukenda @ Tall [43] Muuza Mkaa, mkazi wa Makambako Mkoa wa Njombe, Christopher Burton Mwakanani [37] mkazi wa Tukuyu na Noah Paul [32] mkazi wa Uyole Jijini Mbeya kwa tuhuma za kujihusisha na matukio ya Unyang’anyi wa kutumia silaha katika maeneo mbalimbali mkoani Mbeya.

Watuhumiwa walikamatwa katika maeneo tofauti Mkoani Mbeya, Mkoani Iringa eneo la Ihowanza Malangali na Mji Mdogo wa Makambako Mkoani Njombe. Baada ya mahojiano na watuhumiwa hao walimtaja mtuhumiwa Fabian Francis @ Nsabhi [42] Fundi Seremala, mkazi wa Isyesye Jijini Mbeya ndiye mwenye silaha waliyoitumia kufanya uhalifu, msako ulifanyika na mtuhumiwa huyo alikamatwa ambapo baada ya mahojiano alikiri kuwa silaha hiyo amehifadhi kwenye karakana yake Mtaa wa Hayanga – Sae.

Mnamo Aprili 19, 2025 upekuzi ulifanyika katika karakana ya kutengeneza samani iitwayo “BAMBOO FURNITURE” inayomilikiwa na mtuhumiwa Fabian Francis @ Nsabhi iliyopo Mtaa wa Hayanga – Sae Jijini Mbeya, katika upekuzi huo kulikutwa Silaha moja ya kivita aina ya SKS [Semi-Automatic Rifle] ikiwa na

risasi 28, Maganda ya risasi 02, vipande 02 vya Nondo, Pliers 01, Panga dogo 01, vipande 02 vya msasa na vifaa vingine vya bunduki kama vile Firing pin, magazine flower ambavyo vyote alikuwa amevihifadhi kwenye mifuko ya Nailon na Sandarusi na kufukia ardhini katika karakana yake.

Baada ya mahojiano zaidi alikiri kutumia silaha hiyo kufanya matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha Jijini Mbeya na Mikoa jirani na kuwa tayari kwenda kuonesha baadhi ya mali alizopora ikiwemo simu, mashine za uwakala wa Benki na hazina yake nyingine ya risasi za silaha hiyo, ndipo timu ya Askari iliongozana na mtuhumiwa huyo kwenda kuonesha vitu hivyo alivyokuwa ameficha porini jirani na Shule ya Sekondari Forest Jijini Mbeya. Baada ya kufika eneo hilo, mtuhumiwa alipotaka kuonesha mahali alipoficha vitu hivyo ghafla alikurupuka na kutaka kukimbia ndipo Askari walifyatua risasi tatu hewani kumuamuru asimame lakini alikaidi na kukimbilia vichakani ndipo Askari walifyatua risasi zilizompata kwenye mguu wa kushoto. Baada ya hapo, majeruhi alikimbizwa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya kwa matibabu na baada ya kufikishwa mapokezi, akiwa katika taratibu za kupatiwa matibabu alifariki dunia.

Kwa ujumla, watuhumiwa wote wamekiri kuhusika katika matukio tofauti ya unyang’anyi wa kutumia silaha likiwemo tukio la Aprili 01, 2025 saa 2:00 usiku huko Mtaa wa Masewe Ilemi Jijini Mbeya wakiwa na Silaha ya kivita aina ya SKS walimvamia Mfanyabiashara aitwaye Bakari Albert Mbilinyi [32] akiwa nyumbani kwake na kumjeruhi kichwani utosini na kisogoni na kisha kumpora Begi dogo la mgongoni lililokuwa na mashine tatu za Uwakala wa Benki ya NMB, CRDB na NBC, Simu ndogo 06 aina ya Nokia 2, Tecno 2 na ITEL 2 pamoja na Smartphone aina ya Samsung S32.

Matukio mengine ya unyang’anyi wa kutumia silaha waliyafanya huko Wilayani Rungwe mnamo Aprili 04, 2025 Kitongoji cha Kyimo, Kijiji cha Syukula ambapo walimvamia mfanyabiashara aitwaye Anord John Seleman [23] mkazi wa Kijiji cha Syukula wakati anarudi nyumbani akitokea Kyimo Juu kwenye biashara zake na kumnyang’anya fedha taslimu Tshs.25,000,000/=, mashine tatu za Uwakala wa Benki ya NMB, CRDB na NBC pamoja na simu za mkononi za kufanyia miamala ya fedha zilizokuwa kwenye begi dogo la mgongoni na kutokomea kusikojulikana.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa jamii kuacha kujihusisha na uhalifu ikiwemo matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha na nguvu kwani uhalifu haulipi na hauna nafasi katika jamii. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lipo imara na linaendelea na misako ya nguvu kuwasaka watu wote wanaojihusisha na uhalifu wa aina yote na halitasita kumchukulia hatua kali za kisheria kwa yeyote atakayebainika kuhusika na uhalifu huo. Lengo ni kuhakikisha Mkoa wa Mbeya unakuwa salama.

Post a Comment

Previous Post Next Post