" WASIFU WA ALIYEKUWA MKURUGENZI WA TANESCO, AACHA WATOTO KUMI NA TANO....

WASIFU WA ALIYEKUWA MKURUGENZI WA TANESCO, AACHA WATOTO KUMI NA TANO....

 


“Alikuwa zaidi ya kiongozi alikuwa dira ya maendeleo katika sekta ya nishati.”

Katika taifa linalojenga msingi wa maendeleo kupitia nishati endelevu na miundombinu imara, jina la Mhandisi Gisima Nyamohanga haliwezi kupita kimya kimya. Alikuwa mzalendo aliyejitolea maisha yake kuhakikisha kila kijiji kinapata mwanga, kila mradi wa miundombinu unakuwa na dira, na kila taasisi anayogusa inapata ufanisi wa hali ya juu.



Sasa, Tanzania inaomboleza msiba mkubwa kumpoteza mtaalamu, kiongozi, baba, na rafiki wa wengi.

Mwanzo wa Safari

Marehemu Mhandisi Gisima Nyamohanga alizaliwa tarehe 10 Septemba, 1969, mkoani Mara. Safari yake ya elimu ilianza katika Shule ya Msingi Mlimani, Dar es Salaam, alikohitimu mwaka 1984. Aliendelea na masomo ya sekondari katika Shule ya Azania (1985–1988), kisha Kidato cha Tano na Sita katika Shule ya Kibaha, akihitimu mwaka 1991.

Mwaka 1992 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuhitimu Shahada ya Uhandisi wa Umeme. Aliendelea na masomo ya juu na kupata Shahada ya Uzamili ya Usimamizi wa Uhandisi (2009–2011) na Shahada ya Uongozi wa Biashara (MBA) kati ya 2012–2014. Pia alihitimu shahada ya juu ya sheria za usuluhishi kutoka Chuo cha Ustawi wa Jamii, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Sayansi ya Fedha kutoka chuo kikuu nchini Scotland mwaka 2018.

Kiongozi MwenMaonoye

Mhandisi Gisima alianza kazi mwaka 1996 katika kampuni ya BP Tanzania ambako alihudumu hadi mwaka 2004. Uwezo wake wa kipekee ulimuwezesha kufanya kazi kimataifa, ikiwa ni pamoja na kazi za ushauri nchini Uingereza kati ya 2004–2008 katika kampuni za Business Care Services na ESD Limited.

Miaka yake mingi ya uzalendo ilionekana zaidi aliporejea nchini na kujiunga na Wakala wa Umeme Vijijini (REA) mwaka 2008. Alipanda ngazi hadi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa REA (2016–2019), akisimamia miradi mikubwa ya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya vijijini ambayo yameleta mabadiliko chanya kwa jamii nyingi.


Kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, alihudumu kama Mhandisi Mkuu wa TBA, akisukuma mbele ajenda ya serikali ya maendeleo ya miundombinu. Uteuzi wake kama Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO mwaka 2023 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ulikuwa ushuhuda wa imani kubwa waliokuwa nayo kwake.

Mafanikio Yasiyopimika

Katika uongozi wake TANESCO, Mhandisi Gisima aliongoza mageuzi katika upatikanaji wa nishati, usimamizi wa miradi mikubwa, na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa. Maadili ya kazi aliyoyaishi – uwazi, uwajibikaji, na uadilifu – vilimfanya kuwa kiongozi anayeheshimika ndani na nje ya nchi.

Familia na Maisha Binafsi

Marehemu alikuwa mume mwenye upendo na baba wa watoto 15. Aliacha nyuma wake wawili na familia iliyomtegemea kama nguzo ya upendo, hekima na msaada.

Mwisho Usiyotarajiwa

Ajali ya gari iliyotokea tarehe 13 Aprili 2025 katika Wilaya ya Bunda, Mara, ilikatisha ghafla maisha yake akiwa na umri wa miaka 56. Alikuwa bado na ndoto nyingi, mipango ya maendeleo na dira ya kulifikisha taifa mbele zaidi katika sekta ya nishati.

Tanzania imepoteza zaidi ya mtaalamu – imepoteza mshauri, kiongozi, na mwana wa taifa mwenye maono makubwa. Alama aliyoiacha katika taasisi alizotumikia na mioyoni mwa Watanzania haitafutika.

Bwana ametoa, Bwana ametwaa. Jina la Bwana lihimidiwe.

Post a Comment

Previous Post Next Post