Na Mwandishi Wetu, Tabora
Wakati Bunge likitarajiwa kuvunjwa Juni 27, mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema wabunge ambao hawakufanya vizuri katika majimbo yao wala kurudi kwa wananchi watambue Chama hakitakuwa na namna ya kuwasaidia kwa sababu walipewa nafasi wakashindwa kuzitumia.
Kimesisitiza katika kuhakikisha CCM inapata wagombea ubunge na udiwani wanaokubalika kwa wananchi kimeamua kubadilisha utaratibu wake wa kupata wagombea katika nafasi hizo ili kuhakikisha wananchi wanawapiga kura Chama hicho na hatimaye kushinda Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akizungumza jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Tabora alipokuwa akihitimisha ziara yake katika Mkoa huo, Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira alisema Chama kimebadilisha mfumo katika kupata wagombea udiwani na ubunge kwa kupanua wigo wa demokrasia kwa kuongeza idadi ya wapiga kura.
“Tunataka kazi yetu iwe rahisi maana tunataka mgombea ubunge mwenzetu ambaye pia akienda kwa wananchi ni mwenzao kwa sababu hawezi kusahau kurudi kwa wenzake.
“Kwa hiyo kama mtu ulifanya vizuri huwezi kuwaambia wananchi ulikuwepo. Ulikuwepo sawa lakini kama maoni hayaendi sawa utatusamehe maana tunataka yule ambaye alifanya vizuri, kama hukufanya vizuri sasa tutakusaidiaje?.
“Maana CCM tulikupeleka na kuchaguliwa lakini baada ya kuchaguliwa ukapotea. Umefika wakati wa uchaguzi unasema nimerudi nyumbani, ulikuwa umeenda wapi? Na kama kweli ulisafiri kwa nini hukuwaaga waajiri wako,” amesema Wasira.
Akieleza zaidi Wasira amesema ukweli ni kwamba uchaguzi wa wabunge utakuwepo na umeshafika na mkutano Mkuu Maalum wa CCM uliweka utaratibu wa kupata wagombea kwa sababu Chama lazıma kiwe kinafanya mabadiliko kulingana na wakati.
Amesema wamefanya mabadiliko katika uteuzi na kwamba itakapofika Juni 28, na Julai 5 mwaka huu watakuwa wameshajua nani anagombea na kuongeza wanajua sasa kuna watu wanajipitisha kaika majimbo na kata.
“Sasa hivi tunajua wako wanapita pita tunawafahamu na tunawafuatilia mwenendo wao na hatufuatilii waliopo bali hata wa zamanı maana kuna mambo hatuyapendi sana lakini itakapofika wakati huo tutajua.
“Siku hizi hakuna kupita bila kupingwa sheria imekataa, kwa hiyo hata ukifanya kuzuia wengine unapoteza muda acha waje kama ni 10 au 20. Sio kwamba tunamkoa mtu hata kidogo.
“Tunataka watu wengi wapige kura ya maoni watuambie kwa maoni yao nani anafaa kuwa wa kwanza, wa pili na wa tatu maana huwezi kununua watu 13,000 na ukiwanunua utakufa kabla hujawalipa wote, hutaweza maana zamanı walikuwa wako wachache,” amesema Wasira.
Wasira amesisitiza kuwa, wametaka watu wengi na hasa watu ambao wako karibu sana na wananchi ndio wapige kura ya maoni ili wakija katika uchaguzi wa mwisho mmoja akipitishwa wananchi waseme "kama ni huyo sawa sawa" sio Chama kikipeleka mgombea wananchi wahoji huyu wamemtoa) wapi.
Post a Comment