Jeshi la Polisi Mkoa wa Ruvuma limefanikiwa kukamata vipande 65 vya nyaya za umeme mali ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), ambavyo vilikuwa vimehifadhiwa nyumbani kwa watuhumiwa wawili waliokuwa wakitafuta wateja wa kuviuza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, SACP Marco Chilya, amethibitisha tukio hilo na kueleza kuwa nyaya hizo zimekamatwa kupitia operesheni inayoendelea kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na taasisi mbalimbali za serikali.
Watuhumiwa waliokamatwa ni Idrisa Mnimi (21) mkazi wa Matarawe na Ramadhan Kalumbu (19) mkazi wa Mateka Songea ambao walikamatwa Aprili 11, 2025.
Kwa upande wake, Mhandisi Mashauri Adam akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TANESCO mkoa wa Ruvuma, amesema wizi wa miundombinu ya umeme umekuwa changamoto kubwa kwa zaidi ya miaka mitatu na kusababisha hasara ya zaidi ya shilingi milioni 150.
Ameeleza kuwa nyaya hizo zilizokamatwa ni za shaba na ni sehemu ya miundombinu ya transfoma, zikiwa na thamani kubwa sokoni kutokana na kuwa shaba halisi.
Mhandisi Mashauri amepongeza jitihada za Jeshi la Polisi na kutoa wito kwa wananchi kushirikiana kwa kutoa taarifa kuhusu wahalifu, amesisitiza kuwa uharibifu wa miundombinu ya umeme unazorotesha maendeleo ya jamii na uchumi kwa ujumla.
TANESCO imedhamiria kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kulinda miundombinu yake na kuimarisha huduma kwa wananchi, Pia imetoa rai kwa wakazi wa Ruvuma kutunza miundombinu ya umeme kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Post a Comment