Baada ya tetesi kuenea mitandaoni kuhusu tuhuma za upangaji matokeo katika mechi kati ya Yanga SC na Fountain Gate, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ali Kamwe, amezungumza hadharani na kuweka wazi msimamo wa klabu hiyo.
Kamwe alionekana kushangazwa na kile alichokiita “mchezo mchafu” unaolenga kuchafua jina la Yanga, na alitaka ukweli ujulikane haraka.
Tuhuma hizo zilianza baada ya mechi hiyo kumalizika kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 kwa upande wa Yanga.
Mashabiki na baadhi ya wanamitandao walianza kutupia lawama kwa golikipa wa Fountain Gate, John Noble, ambaye anatokea Nigeria na pia ni sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria.
Noble anadaiwa kufanya makosa kadhaa ya ajabu yaliyopelekea timu yake kufungwa kwa urahisi, jambo lililoibua hisia kuwa huenda mechi hiyo "iliuzwa".
Baada ya mchezo huo, taarifa zilieleza kuwa kipa huyo aliondolewa haraka kambini na hakurejea na timu hotelini.
Zaidi ya hapo, baadhi ya wachezaji wa Fountain Gate walionekana wakionyesha hasira kali, wakihisi kuwa Noble aliisaliti timu yao kwa makusudi.
Inasemekana baadhi yao walitaka hata kumshambulia kwa hasira baada ya mchezo kumalizika.
Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Robert Matano, naye hakusita kueleza maoni yake kwa vyombo vya habari.
Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Matano alieleza kuwa makosa ya Noble yalikuwa ya wazi mno na yamesababisha timu yake kudhalilishwa mbele ya mashabiki.
Alisema kuwa haikuwa kawaida kwa kipa wa kiwango cha juu kufanya makosa kama yale bila sababu ya msingi.
Kwa upande wake, Ali Kamwe alisisitiza kuwa Yanga SC haina uhusiano wowote na matokeo hayo na alitaka mamlaka husika kuchunguza suala hilo kwa kina.
Aliongeza kuwa ushindi wao ni halali na umetokana na maandalizi mazuri ya timu na juhudi za wachezaji wao uwanjani.
Kamwe alitoa wito kwa mashabiki wa soka kuwa na subira na kutopotoshwa na taarifa zisizo rasmi zinazozunguka mitandaoni.
Tukio hili limeibua mjadala mpana kuhusu usalama wa michezo, uadilifu wa wachezaji, na namna Ligi Kuu Tanzania Bara inavyoshughulikia tuhuma za rushwa na upangaji wa matokeo.
Mashabiki wengi sasa wanatazama kwa hamu hatua zitakazochukuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusiana na sakata hili.
Post a Comment