" ZAIDI YA WATU 1,500 KUSHIRIKI KONGAMANO LA 18 LA KIMATAIFA LA ELEARNING AFRICA

ZAIDI YA WATU 1,500 KUSHIRIKI KONGAMANO LA 18 LA KIMATAIFA LA ELEARNING AFRICA

 ZAIDI ya washiriki 1,500 wakiwemo mawaziri wa elimu kutoka zaidi ya nchi 50 za Afrika wanatarajiwa kushiriki katika Kongamano la 18 la Kimataifa la eLearning Africa, linalotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 7 hadi 9 Mei 2025, jijini Dar es Salaam.


Litakuwa jukwaa la kujadili mbinu mbalimbali za kuongeza matumizi ya teknolojia za kidijitali katika elimu na sekta nyingine muhimu.

Akizungumza Aprili 16, 2025 Jijini Dra es Salaam katika harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kufanikisha Kongamano hilo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema kongamano hilo linatoa fursa ya kipekee kwa Tanzania sio tu kujifunza, bali pia kubadilishana uzoefu na mataifa mengine.

Amesema kuwa mkutano huo ni kielelezo cha ukuaji wa diplomasia ya elimu na teknolojia nchini, na utasaidia kuhamasisha uwekezaji mpya.

Naye Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, aliyemwakilisha mgeni rasmi katika kongamano hilo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, ameeleza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu ni “Fikiria upya elimu na maendeleo ya rasilimali watu kwa ustawi wa Afrika.”

Ameeleza kuwa kaulimbiu hiyo inalenga kuangazia nafasi ya teknolojia katika kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi kwa maendeleo ya bara la Afrika.

Ulega amesema kongamano hilo litaambatana na maonesho ya teknolojia ya elimu, huku makampuni ya kitaifa, kikanda na kimataifa yakitarajiwa kushiriki.

Na kwamba itasaidia kuvutia uwekezaji, kuendeleza ubunifu wa teknolojia ndani ya nchi, na kuchangia katika kukuza uchumi wa ndani kupitia huduma na bidhaa zitakazotolewa.

“Matumizi ya teknolojia katika elimu ni jambo lisiloepukika. Mageuzi makubwa yaliyoanza kufanywa na Wizara ni hatua muhimu kuelekea katika mfumo wa elimu unaoendana na mahitaji ya sasa ya dunia,” amesema.

Mkutano huo pia utawakutanisha mawaziri 50 kutoka nchi 49 za Afrika, ambapo watajadili na kuazimia mikakati ya pamoja ya kuandaa nguvu kazi yenye uwezo wa kubuni na kutumia teknolojia za kidijitali kwa maendeleo ya bara.

Amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hilo.

Katika harambee hiyo ya maandalizi, kiasi cha Shilingi bilioni 1.5 kilichangwa na taasisi mbalimbali kutoka ndani ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wizara ya Fedha, ili kufanikisha tukio hilo muhimu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, amesema kongamano hilo litafanyika nchini kwa mara ya pili tangu lilipofanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2011 na kwamba hatua hiyo ni ushahidi kuwa Tanzania ina uwezo wa kuandaa na kuhudumia mikutano mikubwa ya kimataifa.

“Tunamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia ombi la kuwa mwenyeji wa kongamano hili. Uamuzi huu unaakisi dhamira ya serikali katika kuwekeza kwenye elimu na teknolojia, sambamba na kukuza utalii wa mikutano,” amesema Prof. Nombo.

Post a Comment

Previous Post Next Post