Chama kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe (MBCU) kilichopo mkoani Geita kimeliongeza zao la dengu kuwa miongoni mwa mazao yanayosimamiwa na chama hicho.
Mwenyekiti wa MBCU Said Tangawizi amesema kuongezwa kwa zao hilo kwenye Ushirika huo kutaleta manufaa kwa pande zote mbili, yaani kwa mkulima pamoja na chama kwa mkulima kupata uhakika wa soko, lakini chama kitaongeza mapato yake pamoja na idadi ya wanachama itaongezeka.
Amesema MBCU pamoja na mazao wanayojishughulisha nayo ya pamba na tumbaku, kwa sasa wameongeza zao la dengu, na kwamba wamewasisitiza wakulima wa dengu kujiandaa kuingia kwenye mfumo wa stkabadhi ghalani lengo likiwa ni kumsaidia mkulima kupata bei nzuri.
"Sisi kama MBCU pamoja na vyama vya msingi na serikali kupitia mfumo wa stkabadhi ghalani tutakuwa tumepata vyanzo vya mapato kama tukiifanya tukaisimamia vizuri mkulima atapata, sisi tutapata pamoja na serikali kupitia halmashauri" Alisema Tangawizi
Hata hivyo Tangawizi amesema bado MBCU kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika inaangalia namna ya kuliingiza zao hilo kuwa miongoni mwa mazao yanayopatiwa ruzuku ya pembejeo ili kumpunguzia gharama mkulima za kuendesha kilimo cha zao hilo.
Mkulima wa dengu kutoka Rugunga Amcos wilaya ya Mbogwe mkoani Geita Mayeji Sangijo amesema kuingizwa kwa zao la dengu kwenye chama kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe (MBCU), imewasaidia wakulima kupata soko la uhakika na bei nzuri ya zao hilo.
Amesema kwa sasa serikali imelisimamia vyema zao hilo na wameondokana na walanguzi waliokuwa wakimnyonya mkulima awali, japokuwa elimu bado inahitajika kwa wakulima, kwani wapo ambao wanaendelea kuuza dengu kwa walanguzi wanaoingia kinyemela mashambani na kuwadanganya kwa kuwakopesha pembejeo na wanapokaribia kuvuna walanguzi hao wanakwenda kuzichukua dengu kwa bei ya chini.
Amesema ili kuondokana na changamoto hiyo, ameiomba serikali kuliingiza zao la dengu kuwa miongoni mwa mazao yanayopata ruzuku ya serikali ili waweze kuboresha kilimo hicho kulimwa kisasa na wewe mkulima anufaike na jembe lake.
"Tunaomba sisi wakulima wa dengu tuingie kwenye mfumo wa kusaidiwa na serikali kama ni kukopeshwa pembejeo, viuatilifu vinavyohitajika, mbegu nzuri za kitaalam kama ilivyo kwenye tumbaku na pamba" Amesema Sangijo
Amengeza kuwa "Wakulima wetu wakianza kulima watu wenye fedha wanampa mkulima fedha za kulimia, pembejeo na kila kinachohitajika, halafu kwenye mavuno anakuja kuchukua dengu nyingi akisema analipa fedha yake, halafu baadae ndo ananunua kilichobaki kwa bei anayotaka yeye"
Post a Comment